side ads

TUNAMTAKA KIKWETE MWENYE USO WA UKAUZU

Na hapa simaanishi atende kile ambacho hakika kitafanya mbungu zishuke, kwa maana ya kujitoa CCM na kujiunga na kambi ya upinzani. Laa, namaanisha kuwa asimame yeye kama yeye. Yeye kama Jakaya Mrisho Kikwete na awaongoze wananchi ambao wanaonyesha bado kuwa na imani naye.

Ripoti ya utafiti uliofanywa na kampuni ya Synovate, (zamani ikiitwa Steadman Group Tanzania), yenye kuonyesha 81% ya Watanzania wangali na imani Jakaya Mrisho Kikwete, ni kama imepita kimya kimya hivi.

Katika zama hizi ambapo Watanzania tumeonyesha kuwa na mwamko mkubwa katika masuala yenye kugusa utawala wa nchi yetu na hivyo viongozi wetu pia, kimya hiki kwangu mimi kimekuwa ni cha kustaajabia kidogo. Na ingawa zinaweza kutajwa sababu lukuki zenye kuchangia hali hii, lakini kuna kubwa moja ambayo naamini iko wazi.

Na sababu yenyewe ni kuwa, kwa namna yoyote ile, ripoti hii imekuwa RIPOTI POA. Ndio, ingekuwa ya moto, ni wazi kabisa kuwa zisingepita hata saa 24, kabla hatujawasikia waheshimiwa Fulani Fulani ambao kazi yao siku zote ni kukosoa kila kinachomkosoa bwana mkubwa, kuibuka na nadharia nyingi zilizoandaliwa katika mfumo wa mashairi yasiyokuwa na vina wala mizani.

Ieleweke tu hapa kuwa, Jakaya Mrisho Kikwete, ambaye ripoti inaonyesha kuwa nyuma yake kuna 81% ya wananchi ambao wangali wana imani naye, ni Raisi wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa upande mmoja na Mwenyekiti wa chama tawala cha CCM, kwa upande wa pili.

Hii maana yake ni kuwa kwa upande wa chama anachokiongoza, wafuasi wake wamekaa kimya bilashaka wakikenua meno kwa imani ya kuwa “kwakuwa baba anakubalika, basin a familia yake kwa ujumla inakubalika. Na kwa upande wa serikali ambayo yeye ndio kiongozi wake mkuu, vivyo hivyo. Kwa pande hizo zote, ni wazi kuwa ripoti hii ilikuwa ripoti poa. Sasa kwanini waanze kupiga mayowe, wakati watu wameshaiona wenyewe?

Ni katika uelekeo huo huo, uelekeo wa namna hiyo hiyo basi ninaamini kabisa kuwa, zipo sababu nyingi sana ambazo zimewafanya watu kuikalia kimya. Lakini kwa upande wangu, ripoti hii kwakweli si jambo ambalo linaweza kuachwa likapita kimya kimya, kwasababu kuna mengi ninayoyaona nyuma yake.

Kwangu mimi, ripoti hii imekuwa kama sababu na kielelezo kingine chenye kutosha kabisa kumkalisha chini Kikwete, kumfanya awaze na hatimaye afikie mahali pa kuona umuhimu wa kufanya maamuzi magumu pengine kuliko yoyote yale ambayo amewahi kuyafanya katika maisha yake.

Ndio! Katika zama hizi ambazo taifa letu limekuwa likiendelea kutafunwa kwa kasi kubwa na ufisadi, huku wengi wa wanaotuhumiwa wakiwa ni watendaji walioko serikalini lakini ndani ya serikali hiyo hiyo akawepo kiongozi mmoja ambaye wananchi wangali wana imani naye, licha ya kuwa ameshindwa kuchukua hatua kwa watuhumiwa mbalimbali, hili si jambo la kupuuzwa hata kidogo.

Kwamba pia katika zama hizi ambako sehemu kubwa ya viongozi wa chama tawala wamekuwa wakishutumiwa waziwazi kuendekeza vitendo vya rushwa kiasi cha wananchi wengi kuendeleea kupoteza imani nacho hata kule vijijini ambako ndio ilikuwa ngome kuu ya CCM, lakini bado mwenyekiti wake akaonekana kuwa anapendwa na wananchi hao hao, pia si jambo la kulichukulia poa.

Labda tuiweke namna hii. Endapo inatokea familia Fulani watoto wake wakawa wanatuhumiwa mtaa au mji mzima kuwa ndio watoto watukutu, wasiokuwa na utu hata kidogo, kawaida lawama za jamii yenye kuizunguka familia hiyo huelekezwa kwa wazazi au mzazi wa watoto hao. Sasa inapotokea watoto watukutu lakini jamii ina imani na wazazi au mzazi, maana yake ni nini hapo?

Kuna mambo kadhaa ambayo nayaona nyuma ya ripoti ile. Mambo ambayo ninaamini kuwa kamwe mheshimiwa Rais, hatakiwi kuyapuuzia kwa namna yoyote ile. Na jambo la kwanza kabisa ni kwa yeye mwenyewe kujiuliza, ni kwanini ripoti hiyo imekuwa hivyo kwa upande wake, ilhali kutwa kucha, amekuwa dampo la lawama mbalimbali za Watanzania.

Amekuwa akilaumiwa kwa kushindwa kuwawajibisha watendaji mbalimbali ndani ya serikali yake, licha ya kuwa tuhuma ambazo zinawakabili ni za waziwazi na ambazo ushahidi wake hauhitaji wala msaada wa washauri wake ili kuwachukulia hatua. Amekuwa akishutumiwa kwa utawala wake kuwa legelege, linapokuja suala la kuchukua hatua zilizochungu kwa baadhi ya watu lakini zenye manufaa kwa Watanzania.

Na hapa ndipo ninapoanza kuiona au kuichukulia ripoti ile kama kitu ambacho hatakiwi kukiacha kikapita kimya kimya tu. Ninachokiona katika ripoti ile ni ujumbe wa Wana CCM na Watanzania kwa kiongozi wao kuwa umefikia wakati way eye kujipambanua kutoka katika kichaka alimojificha. Ujumbe wa kumtaka ikibidi, afanye maamuzi magumu ya kuhakikisha kuwa taratibu za uchaguzi zinabadilika na kuchukua mkondo mpya.

Ni ujumbe wa kumtaka Kikwete, ajitoe katika makucha ya chama ambacho kimekuwa kikituhumiwa kukumbatia ufisadi. Na hapa simaanishi atende kile ambacho hakika kitafanya mbungu zishuke, kwa maana ya kujitoa CCM na kujiunga na kambi ya upinzani. Laa, namaanisha kuwa asimame yeye kama yeye. Yeye kama Jakaya Mrisho Kikwete na awaongoze wananchi ambao wanaonyesha bado kuwa na imani naye.

Na katika kutekeleza hili, bilashaka ninaamini kuwa umefikia wakati way eye kuhakikisha kuwa ile sheria ya kuruhusu mgombea binafsi, inatekelezwa kwa matendo na si kuendelea kuwa katika makabrasha ambayo huenda yalishaliwa na mchwa huko yalikotupwa.

Ndio, wapinzani mara kadhaa wamemuelezea yeye kama yeye kuwa ni mtu safi. Watanzania nao wamemuonyesha hilo waziwazi kupitia utafiti niliougusia hapo juu. Sasa kwanini basi ashindwe kusimama imara yeye kama yeye wakati anajua kabisa kuwa ana nguvu za kutosha kabisa za kumpa sapoti ya kusimama imara?

Kwanini aendelee kuwa ulimi uliozungukwa na meno ambayo yamejaa harufu chafu? Na ukiachilia mbali ile tabia ya viongozi wetu kuchukulia kila kitu poa, naamini kabisa kuwa hili linawezekana. Inawezekana kabisa kuiona picha ya Jakaya Mrisho Kikwete, katika makaratasi ya kura, akiwania uraisi mwaka 2010, lakini akiwa si kutoka CCM, CUF, CHADEMA nk. Inawezekana. Lakini litatekelezeka? Hapa ndipo ninaposema kuwa naamini anatakiwa kukaa na kutafakari kwa kina.

Lakini kwa upande wa pili, Kikwete, ambaye anaongoza serikali ambayo kashfa za ufisadi zimeiyumbisha kiasi cha kupelekea kubadili baraza lake la mawaziri mwaka juzi, ameendelea kuwa wa kuaminiwa na Watanzania, hili nalo linatuambia kuwa Watanzania wanamwambia kiongozi wao kuwa, wanamuona zaidi ya vile anavyojifahamu.

Wanamuona Kikwete, ambaye ndani yake wanaziona nguvu alizokuwa nazo ambazo anaweza kuzitumia kufanya kila lililo jema kwa Watanzania, licha ya kuwa atawaudhi wachache sana. Wanamwambia kuwa “Tunauona uwezo wako ndani yako na tunataka tuuone ukiutumia kwa maslahi ya taifa lako, wananchi wako na uwafanye wacheke baada ya kulia kwa muda mrefu”

Ndio! Wanachomwambia Kikwete kupitia utafiti ule ni kuwa, aache kutabasamu sasa maana huu si muda wa kutabasamu. Ni muda wa kuuvaa UKAUZU na kusafisha baraza lake la mawaziri. Haijalishi kuwa itagharimu urafiki baina yake na maswahiba yake, maana wao ni wachache kuliko 81% ya watanzania walioko nyuma yake.

Lakini tukirejea tena katika hofu yangu kuu ni kuwa je, atayatekeleza bwana mkubwa au ndio hivyo tena mambo yameenda kimya kimya tu na ameungana na wale wenye kumhadaa mchana akiwa nao, lakini wakawa wasaliti wake wakuu usiku na wakawa wanamuwangia?

Mjadala ni mpana…lakini kwakuwa nampenda raisi wangu, nitaendelea kusema naye kila nitapopata wasaa.

Share on Google Plus

About Rama Msangi

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni: