side ads

ILANI ZA MADHEHEBU NA SERIKALI YENYE KUOGOPA KIVULI CHAKE

WAKATI mchakato wa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, ukitarajiwa kuanza rasmi baadae mwaka huu kwa chaguzi za Serikali za Mitaa, jambo moja ambalo limeshajidhihirisha wazi ni homa ya uchaguzi huo, ambayo imelikumba taifa hivi sasa kiasi cha kusababisha mpasuko wa aina yake.

Kundi la kwanza ndani ya mpasuko huu ni lile la walio madarakani hivi sasa, ambalo kwa wakati huu liko katika kipindi cha presha kupanda na kushuka, wengi wao kwa kujua wazi kuwa wamekalia makuti makavu. Katika kundi hilihili pia wapo ambao wangali katika mshangao wa namna gani miaka imeenda kwa haraka kiasi hiki.

Na kundi la pili katika mpasuko huu, ni lile la wananchi ambao kwa upande wao kuna kila dalili za kuwa wanaelekea kuanza kung’amua thamani yao na ile ya kura zao nyakati za uchaguzi. Kwa kundi hili, hiki ni kipindi cha kujipanga tayari kwa kuonyesha ubavu na hasira zao kwa wale wote ambao waliwapa dhamana ya kuongoza chombo kuelekea kisiwa cha maisha bora, lakini sit u wakafanya kinyume chake, bali wakakizamisha chombo kabisa.

Kundi hili linaelekea kung’amua kwamba, kumbe safari ya kuelekea kisiwa cha maisha bora si rahisi kama walivyotarajia. Ni ngumu zaidi ya maneno. Ni sawa na kupigana vita, na bila shaka ni kupitia mrengo huo, wameamua kujipanga kisawasawa safari hii kwa lengo moja tu, la kuhakikisha kuwa wanashinda vita hiyo, wanaua kila aliye mbele yao mwenye kuonekana adui, wanateketeza kila aina ya kiwazo na hatimaye waweze kufika katika kisiwa hicho.

Ni katika muktadha huu basi ambapo tunashuhudia kuibuka kwa makundi ya watu ambayo kwa makusudi kabisa yameamua kujitwika jukumu la kuwa wachoraji wa raketi zitakazofanikisha ushindi huo. Na hapa nazungumzia madhehebu ya kidini ambayo yamedhamiria kuanza kutoa elimu ya uraia kwa wananchi wake kwa lengo la kuhakikisha kuwa wananchi wanafanya chaguzi hizo kwa mtazamo utakaokuwa wa manufaa kwao.

Tayari wakatoliki wameshatoka na Ilani yao, yenye kupendekeza vipaumbele vya kitaifa, pamoja na Mada za kuongoza maandalizi ya uchaguzi mkuu 2010. Zipi taarifa za waziwazi kuwa Walutheri na Waisilamu nao wako njiani kuja na ilani zao ambazo zitalenga katika kuwaelimisha waumini wao (au Watanzania?) juu ya mambo ya kuzingatia katika uchaguzi huo ili kumpata kiongozi aliye msafi.

Mijadala mingi sana imeshafanywa kuhusiana na Ilani ya Wakatoliki, na si nia yangu kurejea mijadala hiyo, bali kuzungumzia kile ambacho kama mwananchi wa kawaida naweza kuwa nakiona katika mlolongo huu wa ilani za madhehebu ya dini kwa waumini wao.

Kwanza kabisa ni kujisafisha kwa kanisa na viongozi wa kidini kwa ujumla. Ikumbukwe kuwa uchaguzi wa mwaka 2005 ulishuhudia viongozi hawa hawa wakisimama majukwaani na kuwaambia Watanzania kuwa, Jakaya Kikwete, raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alikuwa “ni chaguo la Mungu”

Miaka minne baadae, hivi sasa sio tu kuwa hakuna hata mmoja anayeweza kusimama na kutamka tena maneno kama yale au kuyatetea yale aliyokuwa ameyatamka wakati ule, bali pia wengi wao wanaamini kuwa waliwakosea Watanzania kwa kuwaaminisha kitu ambacho hakikuwa cha kweli. Walikosea utumia makanisa kuwaaminisha Watanzania kile kilichokuwa hisia zao, wakati wakijua kuwa si kweli.

Haiyumkiniki kuwa ndio maana safari hii wameona njia pekee ya wao kuonyesha kujutia makosa yao, ni kutumia vyema busara, akili na nafasi walizo nazo katika kuwafungua macho Watanzania, ili wenyewe waweze kuona chaguo la Mungu na waliweke madarakani, na sio kwa kuelekezwa na wanaojidai kuwa ndio wenye kuona sana.

Ijapokuwa Watanzania wengi hawajaliona hili, pengine niwaeleze tu waliohusika kuandaa waraka ule wa Wakatoliki kuwa, kama watu wazima, tumetumia busara zetu na kubaini kuwa wametumia busara pia katika kutuomba msamaha, na binafsi nimewasamehe kwa uongo waliokuwa wamenisadikisha 2005.

Jambo la pili ambalo ninaliona katika vuguvugu hili la nyaraka, miongozo na ilani za madhehebu ya dini kwa Watanzania, kuelekea uchaguzi wa 2010, ni ishara ya kushindwa kwa serikali ya Kikwete.

Ndio, maana kama ingekuwa haijashindwa na iko sahihi kama ambavyo inatusadikisha pindi makada wake wanapopata fursa za kuzungumza nasi, basi kusingekuwa na haja ya kuwepo kwa miongozo mingine tena ya kuelekea uchaguzi huo.

Nilishangazwa sana na kauli ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliyoitoa Bungeni hivi karibuni kuhusu vuguvugu hili la hizi ilani. Katika moja ya vikao vya Bunge lililokwisha hivi karibuni, siku moja wakati akiwa katika utaratibu aliojiwekea wa kujibu maswali ya papo kwa papo toka kwa wabunge, Pinda, alizungumza maneno yafuatayo (nanukuu)

“…….kama walikuwa na mawazo yao, wangeyatoa kwa serikali na kuona ni mfumo gani utatumika kwa kila dhehebu kuwasilisha maoni hayo kwa nia njema” mwisho wa kunukuu.

Sijui kama Waziri Mkuu alikuwa akimaanisha hayo aliyoyasema kwakweli. Akiwa ameshakiri kuwa amekuwa akishuhudia ilani za namna hiyo sio mara ya kwanza sasa, imenishangaza kuwa wakati wote huo Serikali, na hasa katika wakati huu ambapo yeye ndio mtendaji wake mkuu, ilishindwa kujua kuwa ilitakiwa kuweka taratibu hizo mapema sana.

Hivi Waziri Mkuu anataka kutuambia kuwa kweli serikali hii haijawahi kusikia malalamiko ya wananchi wake kupitia viongozi haohao wa kanisa na madhehebu mengine ya dini hasa kuhusu rushwa na uzozo mwingine ulioigubika serikali katika wakati huu na ikayafumbia macho na masikio? Leo hii bado mnataka kuletewa mawazo ya watu ili muyawekee utaratibu?

Na kama serikali hivi sasa inaona kuwa ilani za madhehebu ya dini zinahatarisha kuligawa taifa kwa misingi ya udini na hivyo kuvunja umoja wetu, kwanini haikutambua nguvu za madhehebu hayo toka mapema wakati yalipokuwa yakiwasilisha malalamiko ya wafuasi wake kuhusu ugumu wa maisha?

Hakika nashindwa kumuelewa mheshimiwa Pinda. Simuelewi kabisaaaaaa. Na nina wasiwasi sana kuwa yeye pia amekumbwa na kizunguzungu kinachotokana na dhamira ya wananchi kuwawajibisha walioko madarakani ambao wamekuwa wakiwasaliti.

Lakini si ajabu. Viongozi wetu wengi ambao kimsingi ni wanasiasa ni wale ambao wamekuwa wakiishi maisha ya maigizo, na sasa linapokuja suala la wao kulazimika kukabiliana na maisha ya uhalisia, inawawia tatizo kubwa sana tu. Na haiyumkini ndio maana kwa wakati huu sehemu kubwa ya watawala wamekuwa wakitumia nguvu kubwa kuanza kutuaminisha kuwa ilani ya wakatoliki ni kosa lenye kustahili kulaaniwa.

Ikiwa serikali hii iliwekwa madarakani na wananchi wake, na wananchi hao hao hivi sasa ndio wamekuwa wakijiwekea misingi au miongozo ya namna nzuri ya kupata serikali zijazo, kuna tatizo gani hapo? Si sawa na mwajiri anapoamua kuweka mikakati mipya ya kuboresha shirika au kampuni yake ili iwe na tija, sasa wafanyakazi wana mamlaka ya kuhoji kweli?
Share on Google Plus

About Rama Msangi

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni: