side ads

TUNDUMA NA KYELA NI MATOKEO YA KIBURI NA DHARAU ZA SERIKALI?

BAADA ya miaka mine ya kuwa kwake madarakani, kuna swali ambalo nimekuwa najiuliza kuhusiana na serikali hii ya awamu ya nne ambayo iko chini ya kamanda wake mkuu mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Je, serikali hii ina tatizo la kiburi na dharau au haijui wajibu wake kwa wale walioiweka madarakani? Au inawezekana pia kuwa inakabiliwa na matatizo yote mawili kwa wakati mmoja?

Matukio mawili ya hivi karibuni mkoani Mbeya, ya wananchi wenye hasira kuvamia vituo vya Polisi na kusababisha hasara kubwa baada ya kuwatuhumu Askari katika maeneo ya Tunduma na Kyela kwa mauaji ya raia wasiokuwa na hatia, yameendelea kuweka mambo mawili hadharani na ambayo ndio msingi wa kuandika kwangu leo.

Kwanza ni ugumu wa utawala katika mkoa huu kwa ujumla, jambo ambalo linatokana na siasa za kuviziana na visasi ambazo zimeonekana kuwa utamaduni wa mkoa huo na jambo la pili linalojipambanua kutokana na matukio hayo mawili, ni kiwango cha kukata tama ambacho wakazi wa Mbeya (kama si Watanzania kwa ujumla wao katika maeneo mbalimbali) wamekifikia.

Itakumbukwa kuwa matukio haya yanakuja katika wakati ambapo mkoa huo ulishajiweka katika kurasa za historia ya aina yake kutokana na tukio la mwaka jana ambako wananchi waliurushia mawe msafara wa raisi Kikwete, wakati alipokuwa katika ziara ya kutembelea wilaya mbalimbali za mkoa wa Mbeya.

Kwa waliofuatilia tukio la mwaka jana, watakumbuka vyema jinsi ambavyo siasa za ajabu ajabu ziliingizwa katika tukio lile hali ambayo ilikuja sababisha kuibuka kwa majibu ambayo yalikuwa ya kujichanganya changanya baina ya wale waliotakiwa kutujulisha ni nini hasa kilijiri.

Tulielezwa wakati ule kuwa waliofanya vile walikuwa wananchi waliokuwa na hamu ya kumuona raisi wao lakini wakashindwa hivyo mawe yale yalikuwa ishara ya kuonyesha hasira za kutokumuona raisi wao. Tukaambiwa pia kuwa walikuwa wahuni tu ambao walijikusanya mahali pale kwa ajili ya kuuchafulia msafara wa raisi.

Zilienea pia porojo za hapa na pale mitaani zikidai kuwa tukio lile lilikuwa limepangwa na baadhi ya wanasiasa ambao walikuwa na lengo la kumchafua mkuu wa mkoa wakati ule wa ziara ya raisi, ili mkuu wa mkoa apokonywe ulaji wake… na blah blah nyingi tu. Kwa ujumla wake katika tukio lile, serikali kuanzia ngazi ya juu hadi ya mkoa, ilijitahidi sana kuonyesha usanii wa hali ya juu. Bahati mbaya sana haikujua kuwa inafukia moto kwa kutumia nyasi kavu.

Na sasa yanapokuja haya ya Tunduma na Kyela, na kuangalia matukio ambayo yaliambatana na matukio hayo makuu ya uvamizi wa vituo vya Polisi, ndipo unapobaini kuwa kuna kitu ambacho ni zaidi ya tatizo kwa serikali yetu tuliyonayo madarakani. Na bahati mbaya sana, nadhani hadi sasa yenyewe imeshindwa kujua kuwa ina tatizo, achilia mbali kutibu.

Malalamiko kuhusu utendaji mbovu wa jeshi la Polisi nchini, ni tatizo ambalo limekuwa la muda mrefu sana. Nathubutu kusema kuwa tatizo la utendaji mbovu wa Polisi, baadhi ya nyakati ndilo ambalo limeiangushia mahakama katika lawama ya uwajibikaji mbovu hasa linapokuja suala la kuachiwa kwa watu wenye tuhuma mbalimbali wanapokuwa wamekamatwa na kufikishwa katika mamlaka husika kwa ajili ya kuchukuliwa sheria.

Kuna baadhi ya nyakati ambapo nimekuwa nikijiuliza kama jeshi la Polisi linafanya kazi zake kwa kufikiri, kupiga ramli, kufuata manuni na sheria, kuzingatia busara, uwazi na ukweli au vipi. Maana baadhi ya mambo ambayo yamekuwa yakifanyika nathubutu kusema ni ya ajabu sana.

Mtu aliyekuwa analiliwa na wakazi wa Tunduma, alikuwa ameuawa kwa kupigwa risasi. Na jeshi halikuwahi kukanusha juu ya kifo cha mwananchi huyo kutokana na kupigwa risasi. Lakini mambo ambayo yalielezwa na mamlaka za Kipolisi juu ya tukio lile kwa wakati ule, yalikuwa ya kushangaza kwa kiasi Fulani kwa upande wangu.

Yalikuwa mambo ambayo ndio yalinirejesha katika kuwaza kwa kiasi gani serikali yetu imejawa kiburi na dharau kwa wananchi walioiweka madarakani. ndio, tilielezwa wakati Fulani kuwa eti mwili ulikuwa ukifanyiwa uchunguzi zaidi. Hii kama haikuwa ishara ya dharau ni nini hasa?

Mtu kapigwa risasi, jambo hilo liko wazi, Polisi hawakanushi, sasa uchunguzi ulikuwa kwa ajili ya kujua nini? Hivi risasi ni nyoka kuwa hadi kuchunguza mwili kujua aina ya sumu au aina ya nyoka aliyemng’ata mhusika hadi kufa?

Kwangu mimi, hii ilikuwa ishara ya dharau kwa wananchi kwa ujumla. Ambao walichukuliwa kama wajinga Fulani ambao wakiambiwa kitu Fulani basi wanatakiwa kukaa kimya na maisha yakaendelea kana kwamba hakuna lililotokea.

Na kama si dharau basi ndipo ninapokuja katika tatizo la pili ambalo ni wazi kuwa nalo linaikabili serikali hii. Kutojua wajibu wake kwa wananchi wake walioiweka madarakani. ndio, kama mwananchi kapigwa risasi, Polisi hawakanushi, maana yake ni kuwa wanakubali hilo kutokea. Na sasa wanapokuja kutuambia kuwa marehemu anachunguzwa zaidi, ni kutuambia kuwa hawajui cha kufanya.

Kwasababu kama wangelikuwa wanajua cha kufanya, wangevaa ujasiri na kusimama mbele ya walioipa dhamana na kukiri kuwa kuna mapungufu makubwa katika utendaji wa Jeshi, yenye kupelekea matatizo kama hayo na hivyo hatua kali zinaanza kuchukuliwa kwa watu wachache wenye matatizo ndani ya jeshi ili kulisafisha.

Halikuwa suala la kujibu kisiasa wala halikuwa suala la kuwafanya wananchi hawajui mapungufu hayo. Halikuwa pia suala la kuwaona wananchi kama watu ambao hawana ukomo wa uvumilivu. Na bilashaka ndio maana muda mchache baadae, tukio kama hilo likajirejea tena mjini Kyela.

Haihitaji mtu kuwa msomi wa chuo kikuu kuweza kugundua kuwa kama tatizo la awali la Tunduma lingekuwa limeshughulikiwa kikamilifu na kwa mujibu wa kilio cha wananchi ambao wamekuwa wakililalamikia jeshi muda mrefu, tusingeshuhudia tena tukio kama hilo Kyela.

Na wala haihitaji mtu uwe na tunguli kuweza kubashiri kuwa matatizo kama hayo hayataishia hapo ikiwa hadi sasa hakuna cha maana ambacho kimeweza kufanywa kwa ajili ya kuonyesha kuwa kuna juhudi za wazi za kulikabili tatizo la udhaifu wa kiutendaji ndani ya Jeshi letu.

Na hapa ndipo ninapojiuliza swali gumu zaidi la; Je, kiburi, dharau vinavyoonyeshwa na serikali yetu vikichagizwa na kufunga kwao macho na kuziba masikio kutosikiliza vilio vya wananchi wake vinatupeleka wapi?

Share on Google Plus

About Rama Msangi

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni: