side ads

MACHAFUKO AFRIKA KUSINI, MATOKEO YA ILANI NA POROJO HEWA ZA VIONGOZI BARANI AFRIKA

Kuanzia mapigano ya wenyewe kwa wenyewe hadi umasikini uliokithiri. Magonjwa ya milipuko, uduni wa miundo mbinu na shida za kila aina; bara la Afrika kwa ujumla halijawahi kuwa na wakati ulio bora kwa watu wake.

Kusini mwa bara hili na hususan nchini Afrika Kusini, wiki hili, kumeshuhudiwa machafuko yenye kuhusisha mamia ya wananchi waliokata tamaa dhidi ya wawekezaji, wengi wao wakiwa ni wakigeni.

Vyombo mbalimbali vya habari ambavyo vimekuwa vikifuatilia machafuko hayo, vimewanukuu wananchi kadhaa wakielezea sababu iliyowasukuma kufanya fujo hizo kuwa ni kutoridhishwa kwao na utekelezwaji wa ahadi za kuboreshewa maisha yao.

Wanamlaumu waziwazi rais Jacob Zuma kwa kutoonyesha jitihada za wazi na zenye kuonekana katika kuwakomboa Waafrika Kusini toka katika ukosefu wa ajira, huduma muhimu za kijamii za afya nk.

Na malalamiko yao yamejengwa katika msingi wa kwamba zilikuwa ni ahadi za bwana Zuma alizozitoa wakati anawaomba wamuingize madarakani jambo ambalo wao wananchi walilifanya. Walimpa kura, zikampa ushindi na sasa yuko Ikulu.

Na sasa wanaona ni wajibu wa raisi wao nae kutimiza ahadi zake alizozitoa kwao. Kuwaboreshea hali ya kiuchumi, kuwatengenezea vijana nafasi za ajira, kuboresha sekta za afya na huduma nyingine za kijamii. Ndio, ahadi si ni deni bwana?

Katika bara ambalo asilimia kubwa ya watu wake hawajaelimika, wachache walioelimika wakiwa ndio hao wanaopewa dhamana za uongozi na kasha wakaanza kutumia ujinga wa wanaowaongoza katika kujinufaisha wao wenyewe, yanayotokea Afrika Kusini, si ya ajabu.

Si ya ajabu kwakuwa imekuwa ni kawaida kwa watawala wengi barani humo kujinufaisha kutokana na mtaji huo wa umbumbumbu wa sehemu kubwa ya watu wake, kwa kuwalundikia ahadi kemkem kupitia kile kinachoitwa ILANI ZA UCHAGUZA.

Hata hivyo, imekuwa ni bahati mbaya sana kuwa sehemu kubwa ya ilani hizo imekuwa ni ile isiyotekelezeka. Imekuwa ikiwashinda wenye kuziandaa kuzifanyia kazi kwakuwa ndani yake zimejaa usanii wa hali ya juu.

Na hata pale kwenye chembe za uhalisia, utekelezaji wake umekuwa ni mgumu kwakuwa maeneo hayo yanakuwa si ya vipaumbele vya wakubwa. Matokeo yake hali za wananchi zimeendelea kuwa duni na za kukatisha tamaa.

Mbaya zaidi si tu kuwa wanashindwa kutimiza ahadi zao bali pia kupitia mtaji wa ujinga wa sehemu kubwa ya wananchi wao, watawala hao hugeukia upande wa kuwahadaa wananchi, kutoa rasilimali zao kama zawadi kwa mabwana wakubwa wa ulaya na kwingineko wanakoenda kufanya ziara zao wakijiwekea mazingira mazuri ya watakako kimbilia wakimaliza kuharibu makwao.

Tukirejea katika taarifa za vyombo vya habari vinavyofuatilia matukio ya Afrika Kusini, vilimnukuu mmoja wa mawaziri wa taifa hilo akidai wanafanya uchunguzi wa chanzo cha machafuko hayo. Na kwamba hatua zitachukuliwa.

Kauli nyingine yenye kuonyesha wazi jinsi gani wale wanaoitwa viongozi, hupenda kuwahadaa wananchi kwa kigezo kilekile cha kwamba wao ni wasioelimika.

Wananchi Afrika ya Kusini na kwingineko ambapo matatizo kama haya hujitokeza, wanabainisha waziwazi kuwa wanafanya hivyo kwakuwa kile walicho au wanachoahidiwa, sicho wanachotendewa. Na katika baadhi ya sehemu hali sio tu kwamba haiboreshwi, bali hudorora hata kuliko ilivyokuwa kabla ya ahadi.

Katika muktadha huo, ni wazi kuwa tatizo sio wananchi, wala pia si suala la kukaa kufanya uchunguzi, kwakuwa liko wazi tatizo lenyewe. Ni kutotimizwa kwa ahadi walizoahidiwa. Tatizo ni watawala wenye kutoa ahadi wasizozitimiza.

Na hasira zaidi za wananchi zinatokana na ukweli kuwa, ahadi zitolewazo huzingatia uwepo wa rasilimali za kutosha katika maeneo yao, lakini ambazo hatimae hazitumiwi kuwaletea tija kimaisha. Bali kuchukuliwa na kupelekwa nje ya nchi tena kwa mtaji wa nguvu za wanachi hao hao.

Kwa mantiki hiyo basi, wananchi wanapewa ahadi wasizotimiziwa, wanapodai haki yao, wanaanza tena kuchunguzwa wao na hatimae wengi wao kukamatwa na viongozi haohao waliowapa mamlaka kutokana na ahadi walizopewa bila kutimiziwa.

Ni kama mgonjwa anayeahidiwa tiba lakini asipewe. Anapolalamikia maumivu kumzidia, madaktari wanamsingizia tena ugonjwa mwingine wa kutokuwa na akili timamu.

Haiyumkini ndio maana machafuko katika Afrika ya Kusini hayatarajiwi kwisha hivihivi bila damu kumwagika. Maana wanyonge wataendelea kudai haki yao, ilhali wakubwa wakikwepa kutimiza wajibu wao na badala yake kutumia nguvu nyingi katika kuwadhibiti wanyonge.

Watawachunguza, watawabaini baadhi na kuwasingizia ndio waanzilishi wa fujo, watawafunga, watawatesa, hilo litazidisha chuki baina ya watawala na wanaotawaliwa. Matokeo kila mahali patawaka moto. Moto ambao kuzimika kwake itakuwa vigumu. Moto wa kudai haki.

Na kwakuwa nguvu ya wengi ni nguvu isiy√łgopa chochote, wanadhani watawadhibiti wote kwa kuwafunga, kuwatesa au hata kuwaua? Hapana. Hawatoweza.

Njia muafaka ni kwa viongozi kukiri mapungufu yao, waache usanii, watimize ahadi zao. Na kama zilikuwa geresha, wakiri na kuwaomba wananchi wawaongoze.

Mungu ibariki Afrika
Share on Google Plus

About Rama Msangi

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni: