side ads

BUNGE LETU HALIAKISI UHALISIA WA MAISHA YETU

Nimesoma, kusikiliza na kuona karibu kila kinachoendelea kutoka mjini Dodoma, ambako Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limekuwa likiendelea na vikao vyake na kwa hakika, nimejiridhisha pasi na shaka kuhusu somo la makala yangu hii. Ndio, Bunge letu haliakisi hali halisi za Watanzania.

Niliwahi kuandika huko nyuma na leo hii nitarejea nilichowahi kukiandika huko nyuma, tena kwa herufi kubwa kabisa kuwa “SINA MASHAKA WALA MATATA YOYOTE YALE KUHUSIANA NA MAMLAKA, WAJIBU, HAKI NA CHOCHOTE KILE KINACHOHUSIANA NA BUNGE LETU, KWA MUJIBU WA KATIBA”. Lakini nina mashaka na wasiwasi wa hali ya juu sana juu ya watu ambao wamepewa dhamana ya kuunda chombo hiki.

Hivi wale Wabunge ambao wamekuwa wakiendelea na vikao vyao pale Dodoma hivi sasa, ni wale ambao tuliwachagua sisi kweli? Ni wale wale ambao mwaka 2005 walikuwa marafiki zetu? Ni wale wale ambao walitupigia magoti na kutusalimia wakati ule? Ni wale wale ambao tulikuwa tukipigana nao vikumbo katika usafiri wa pamoja huku mitaani tunakotoka?

Hivi wabunge hawa ndio wale wale ambao walisema kuwa wamedhamiria kutuletea maisha bora kwa kila Mtanzania? Hivi wametuonyesha kuwa hatukufanya makosa kupanga foleni ndeeeeeefu na kuwapigia kura wakati ule? Hivi wangali wanaabudu usemi wao wa ule wa wakati ule wa kwa pamoja tunaweza?

HAPANA. Binafsi sijaona kama kuna swali ambalo linastahili jibu la NDIO miongoni mwa hayo niliyoyaorodhesha hapo. Labda kwa wateule wachache sana wengi wao wakiwa ni wategemezi wa hawa wanaojiita Wabunge wetu. Ndio, kipi hasa ambacho naweza kukijibu kwa kusema NDIO hapo ilhali hakuna hata moja ambalo nimeweza kuliona miongoni mwa yale waliyokuwa wameniahidi wakati ule?

Hali ya uchumi imezidi kuwa mbaya sana. Maisha yanazidi kuwa magumu kila kukicha, usanii umezidi kukua kila kukicha, uhaba wa masoko bado ni kitanzi kwa Watanzania wenye kufurukuta kujiajiri, kiburi cha viongozi kimezidi kukua kwa kadiri miaka inavyozidi kusonga mbele, dharau nazo zimekuwa zikichukua uelekeo huo huo. Sasa kipi ambacho kinaweza kunifanya niwape tano?

Ukiangalia kile ambacho kimekuwa kikiendelea kule mjini Dodoma, utabaini tena kwa haraka mno kuwa ni kama mchezo wa kuigiza. Maswali mengi yamekuwa ni yale yale ya enzi na enzi na majibu yake yameendelea kuwa yale yale kuwa serikali inajipanga. Bunge limeendelea kuiomba serikali, kana kwamba hiki ni chombo ambacho survival yake inategemea kufurahi kwa wakubwa walioko serikalini.

Na hata pale ambapo pamekuwa na maswali ya maana sana, ambayo ni machache sana hata hivyo, majibu yameendelea kuwa yale yale ya kisanii. Majibu mepesi kwa maswali magumu. Pale ambapo wahusika walijitahidi sana kutaka au kuthubutu kutoa majibu ya maana, basi haikuwa kwa ajili ya waliompigia kura, haikuwa kwa ajili ya Watanzania, bali kwakuwa UCHAGUZI UNAKARIBIA HIVYO WANAHOFIA KUHUKUMIWA NA WANANCHI WAO. Ndio, si wanatamka wenyewe?

Sasa niwape tano kwa lipi hasa? Kwakuwa wanajidai kuniogopa sasa hivi kwakuwa mwakani wanaogopa nitawahukumu? Yaani wameninyonga kiasi hicho na sasa wanataka kunipaka mafuta kwa maneno ya kuonyesha wananiogopa ili niwaonee huruma? HAPANA.

Yale mamilioni ya ajira ambayo tuliahidiwa, sijui hata ni kina nani ambao walau walikumbana na upepo wake? Wakulima wangali wanapigika kama hawana thamani ndani ya nchi yao, kama hawana chochote cha kuchangia katika taifa hili. Je, kuna cha kuwasukuma waipe tano serikali hawa wanaoitwa Wabunge wao?

Safari ndio kwaaaaaanza inaanza.

Share on Google Plus

About Rama Msangi

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni: