side ads

WAWEKEZAJI WA KICHINA: waraka wangu kwa Koero Mkundi

Mpendwa dada, natumai hujambo. Mimi na familia yangu pia hatujambo na namshukuru Mungu kwa kunipa uzima hadi wakati huu ambapo baada ya siku nyingi kidogo za kutowasiliana, nimeona nikukumbuke kwa njia ya barua.

Je, dada, unaikumbuka ile makala yako uliyoandikaga kule katika kijiwe chako cha VUKANI, kuhusu hawa wawekezaji wa Kichina wanaoendelea kufurika nchini? Naamini wewe na wasomaji wako, mngali mwaikumbuka makala ile uliyoipaga kichwa cha “WENZETU WAMEWAKATAA….”, na ni makala hii ambayo leo hii imenisukuma kukuandikia.

Hivi karibuni nilifanya safari ndefu kidogo ya kutoka Mbeya kuelekea Tanga, na wakati narudi nikapitia jijini Dar es salaam, ambako nilionelea kuwa ingekuwa rahisi zaidi kuunganisha safari ya kurejea Mbeya, na ni katika safari hiyo ya kurejea Mbeya tokea Dar, ndiko nilikokutana na mambo ambayo yalinikumbusha kuhusu wawekezaji wa Kichina.

Nilisafiri na basi linalojulikana kwa jina la New Force Enterprises. Mabasi ya kampuni hii ni miongoni mwa mabasi ambayo yamejizolea umaarufu sana hapa Mbeya, kutokana na ukweli kuwa ni mabasi yenye kumilikiwa na kampuni ya Kichina, na ambayo yalianza kutoa huduma zake katika wakati ambapo mjadala kuhusu uwepo wa bidhaa feki za Kichina nchini, ukiwa umetawala nchini.

Naamini unaweza kufikiri ni kwanini nilivutika kutumia huduma za basi/kampuni hii na kwakweli, toka mwanzo wa safari nilikuwa na shauku kubwa sana ya kujua mambo kadhaa kuhusu basi lile na udadisi wangu huo kwa hakika ulinipa mambo mengi sana ambayo yaliibua maswali mengi kichwani mwangu.

Itoshe tu kusema kuwa, ukiachilia mbali ya watu waliokuwemo ndani ya basi lile, vinywaji na viburudisho kama biskuti na pipi, kila kilichosalia kutoka katika orodha hiyo, kilikuwa ni cha kichina. Na nikiri tu kuwa, nilifurahishwa sana na huduma nilizokutana nazo mle ndani, ukiachilia mbali tatizo la mwendo kasi lililonifanya nisafiri roho juu muda wote. Na hili pengine lilitokana na kuwa dereva hakuwa mchina.

Lakini ukiachilia mbali yote hayo, jambo kubwa lililonivutia zaidi katika safari hiyo, ilikuwa ni burudani ya filamu na muziki ambao ulikuwa ukionyeshwa katika luninga ya ndani ya basi hilo, au hata muziki uliokuwa ukipigwa baadhi ya nyakati luninga ile ilipokuwa imezimwa. Vyote vilikuwa vya kichina.

Hebu jenga picha hapo. Safari zaidi ya km 800, unaangalia au kuburudika na burudani za kichina!! Hili lilinivutia sana. Maana lilinifanya nianze kufikiria mikakati ya hawa jamaa katika kutumia fursa ya kutangaza utajiri wa utamaduni wao, vivutio vya utalii na hata muziki na mavazi yao, kupitia fursa chache ambazo tumewapa tena huku tukiwanyanyasa na kuwasema kila kukicha.

Unajua kibinadamu, ni kuwa ukiachilia mbali kifo na ugonjwa labda, mengine yaliyoko humu duniani ukiyaona kwa muda mrefu huwa unayazoea na baadhi yake huanza kukuvutia. Kwahiyo ni wazi basi kuwa, hata kama mwanzo wa safari ile hakuna aliyekuwa na interest na kilichokuwa kikionekana kwenye luninga au kusikika kwenye redio, kuna wakati walilazimika ku-concentrate katika yale na kuvutiwa na walau moja au mawili hivi.

Kiukweli, muda wote wa safari nilikuwa nimetega masikio kusikiliza nini kitasemwa kuhusu burudani zile, na wakati Fulani tulipofika Iringa, kuna muziki ulikuwa unaendelea na ukakatika luningani, ambapo baadhi ya watu walipiga kelele za kuhamaki. Na hapo nika-proove kuwa kuna watu wamevutika.

Nikashusha pumzi, nikaanza kujiuliza maswali kadhaa hivi. Je, ni wangapi ambao wameshasafiri na mabasi haya toka yaanze? Ni wangapi ambao wameshakuwa wanachama regular wa huduma za kampuni hii? Ni kwa kiasi gani wameathirika na burudani za namna hiyo wanazokutana nazo mara kwa mara? Definitely, ni wengi na mara nyingi.

Maana yake hapo ni kuwa tayari kuna kundi la Watanzania ambalo limeshaanza kuhamasika na utamaduni wa wenzetu hawa, wameshaanza kuvutika na burudani zao, kupenda miziki na filamu zao, na bilashaka, kama hawajaanza kuchangamkia kaseti, CD na DVD za kichina, basi ni suala la muda tu, kwani ni lazima wataanza. Na ni wangapi ambao wameshaanza kuvutiwa/kutamani kutembelea nchi hiyo wakati Fulani katika maisha yao? Bilashaka wapo na ni wengi tu.

Maswali yangu hayakuishia hapo. Niliendelea kujiuliza maswali yafuatayo:- Je, hivi sisi tumekuwa tukitumia sehemu na vyombo vya usafiri kwa kiasi gani kutangaza utamaduni, burudani, urithi na utalii wan chi yetu? Je, ikifikia siku jamaa hawa wakaanza na kutoa viburudisho kama biskuti, soda, maji na hata pipi kutoka nchini mwao, tutakataa kweli wakati huduma za usafiri wao tumeshazipenda?

Je, kwa uzembe wa madereva wetu, ikitokea wakasababisha ajali kwa mabasi ya Kichina, na wakaamua kuwa waweke madereva wenye asili ya kwao, tutaweza kuwazuia kweli? Na wakipanua zaidi huduma zao wakaona kuleta madereva inakuwa gharama wakafungua na vyuo International vya Driving, wakaleta wanafunzi toka kule kwao, wasomee udereva hapa hapa nchini na kuchukua kazi za udereva, Watanzania tutalalamika kuporwa ajira na wachina?

Uh!! Nishushe pumzi kwanza dada naaa…… loh!! Kumbe barua yangu imeshakuwa ndefu kama risala ya mwanasiasa!! Basi naomba niishie hapa, nikiamini kuwa maswali mengine nawe utakuwa umeshayatengeneza kichwani mwako, na ukipata muda, bilashaka utanijulisha maswali yako, majibu yake pamoja na majibu ya maswali ambayo yalinisumbua mimi kichwani mwangu.

Wasalaam
Wako kaka yako
Mchambuzi
Share on Google Plus

About Rama Msangi

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni: