side ads

Hatuna haja na vichwa kama hatuwezi kufikiri

Dakika chache sana kabla sijaandika makala hii, nilikuwa nachat na dadangu Yasinta Ngonyani, bloga mwenye kuendesha blogi ya MAISHA. Katika mazungumzo yetu hayo mara tukaangukia katika mada ya mashindano ya urembo ambayo katika miezi kama hii, ndio wazimu wake unakuwa umeiteka Tanzania.

Tukajadili mengi japo kwa ufupi ufupi sana, na akanielekeza katika blogi ya MATONDO, ambako huko nilikutana na makala hii, kuhusu mashindano ya urembo. Maongezi baina yangu na dada YASINTA, pamoja na makala ya MATONDO, vikanirejesha katika jambo moja ambalo limekuwa likiniumiza kichwa kwa muda mrefu. Kiwango cha matumizi ya akili, fikra na kujithamini kwetu.

Nimekuwa nikijiuliza mambo hayo kutokana na mambo ambayo nimekuwa nikiyashuhudia kupitia mashindano haya ya urembo pamoja na wale dada zetu wacheza show wa bendi mbalimbali hapa nchini.

Imeshajengeka hivi sasa kwamba, katika mashindano ya urembo ni lazima dada zetu wavae nguo ambazo zamani zilikuwa zikiitwa za siri, kabla ya kuanza kuitwa za ndani hivi karibuni. Limekuwa jambo la kawaida sana hivi sasa kuwaona wale dada zetu wacheza show wakicheza wakiwa na vivazi vya aina hiyo hiyo. Kifupi ni kuwa, limekuwa jambo la kawaida kwa wacheza show na mamiss, kuvaa au sijui kuvalishwa mavazi yenye kuacha miili yao uchi kwa zaidi ya asilimia 70.

Kinachoniumiza kichwa hapa ni kwamba, hivi ni kwanini wacheza show wakaamua kufanya au kukubali kulazimishwa kuvaa mavazi yale? Hivi, kama wacheza show wa bendi zote wakiweka msimamo na kuwa wanavaa mavazi ya kiheshima zaidi, wapenzi wataacha kwenda kutizama na kuburudika na muziki wao? Na kama kina dada hao wacheza show wenyewe au wanawake kwa ujumla wao hawataki kulishikia hili kidedea na kuona wanajidhalilisha, nani awasaidie?

Vivyo hivyo kwa wanaoshiriki mashindano ya urembo? Ni lazima wavae mavazi ya vichupi? Ni lazima wajiache wazi ndio waweze kuonyesha urembo wao? Je, wakigomea udhalilishwaji wa namna ile, wizara yenye kushughulikia masuala ya kina mama ikaweka sheria kali za kukataza mavazi yale, ni nani atawatikisa? Kwanini tutumie kigezo cha kuwadhalilisha kina dada kwa ajili ya kuwapatia kipato?

Mjadala huu ni mrefu kidogo, ila kwa leo, hebu tuanze kutafakari kwa kupitia hapa. Mzee wa CHANGAMOTO, naye aliwahi kuligusia hili kwa kuandika HIVI:
Share on Google Plus

About Rama Msangi

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

2 maoni:

Yasinta Ngonyani said...

Mjadala huu inabidi uwekwe wazi kabisa kwani sio peke yako ambaye unaumiza kichwa. Na unajua mabaya zidi ni kwamba sasa watoto wetu au niseme taifa la kesho nao wanaiga hivyo. Yaani kwanini nasema hivi ni kwamba hao akina dada wanapovaa hivyo vyupi wanaonekana jinsi walivyo. na wanakuwa hivyo kwa kujinyima kula WANATESWA AU KUJITESA ili kuwa wembamba. Halafu nso wanasema eti ni mrembo. Ule utamaduni wetu wa kuwa akina mama wawe na mwili umekwenda wapi. Nakubaliana na Matondo ni kwamba tunaiga mno kila kitu hata visivyotakiwa kuiga. Na mbaya zaidi nadhani tunaiga bila hhata kufikiri. Kama kuna mtu au IDARA ya wanawake kwa nini wanakaa tu na kufurahia hili jambo. Kwanza ni kwa nini kuwe na miss, fulani. Na kwa nini kusiwe na mrs Fulani Je? ma-Mrs si warembo? kwa kweli inasikitisha sana. naacha nasubiri kinachoendelea

Mzee wa Changamoto said...

Well! Kutaka kuwa tusivyo ni tatizo. Nisingeona tatizo kama ingekuwa ni mavazi ya kawaida, lakini kwa kuwa hawaonekani kufurahia wavaavyo zaidi ya "kazi." Hatuwezi kubisha kuwa wazazi wa kale walivaa hivyo ama zaidi ya hivyo, lakini ilikuwa ni sehemu ya maisha. Kama Dada zetu wangekuwa wako huru kuvaa namna hiyo hata wamalizapo shows zao, wamalizapo mashindano ya urembo na kuanza kupuyanga mitaani na "vivazi" vyao, ningeona sawa. Lakini yaonesha kabisa kuwa huo ni uvaaji wa KUTAFUTA MASLAHI.
Niliwahi kuandika kuhusu Changamoto hii kwenye maisha na visingizio mbalimbali tunavyokuwa navyo kuhusu muziki kwa kusingizia lugha, mavazi na hata kumbi kitu ambacho si kweli ( Bofya http://changamotoyetu.blogspot.com/2009/01/changamoto-yetu-sanaani.html kwa machache)lakini siasa zimeingiliwa na pesa na zimeingilia mfumo wa maisha mpaka ya kiroho.
Bila wenye kutenda haya kuamka, siasa haitamuamkia yeyote.
Mada njema sana.
Blessings