side ads

MALECELA KAZUNGUMZA, HEBU TUZUNGUMZE NAYE BASINiliwahi kuandika siku za nyuma kuhusu Dk. J. S. Malecela, mmoja kati ya magwiji wa siasa za kimedani nchini Tanzania, katika makala niliyoipa kichwa cha “Malecela, usipompenda kwa matendo, utampenda kwa misimamo yake”, na niliwahi pia kuandika wakati wa nyuma kuhusu tofauti kati ya KUZUNGUMZA NA KUSEMA, na bilashaka, leo hii wakati naandika tena kumhusu Dk. Malecela, si mbaya tukakumbukia makala hizo kupitia hapa na hapa.

KUNA msemo unaosema eti tafsiri ya kitu, ni vile mtu anavyokiona au kukichukulia kitu hicho. Naukumbuka msemo huu leo hii ninapotafakari kilichozungumzwa na mzee John Samwel Malecela, hivi karibuni kuhusu Chama cha Mapinduzi, kuwa bado ni chama cha wakulima na wafanyakazi, katika nchi hii.

Kama kuna mtu ambaye hakunielewa niliposema hivi sasa, kila Mtanzania, yuko kama amemwagiwa petrol, akisubiri yeyote akatize tu mbele yake (hata na kipisi cha sigara), ili alipuke, bilashaka, atatakiwa afuatilie sana kile alichokisema John Samwel Malecela, kuhusu CCM, na huenda akanielewa, maana mengi sana yamejadiliwa, yakageuzwa huku na kule na hatimaye baadhi wakafikia suluhisho kuwa, huyu mzee sio bure, ana lake jambo.

Ni kweli, kwa mambo yanavyoendelea ndani ya CCM hivi sasa, na kwa mzee Malecela kutamka maneno kama yale, kwa hakika ana lake jambo, lakini ni lipi hilo jambo lake? Hapo ndipo kila mtu amekuwa na lake la kusema, lakini kwa bahati mbaya sana, nathubutu kusema kuwa, ama hakuna hata mmoja ambaye amemuelewa vizuri mzee Malecela, na kama wapo, basi wamemuelewa au kumsoma vibaya.

Pengine kabla ya kuendelea, nikupe kisa hiki kilichokuwa kikiwahusisha jirani zangu wawili ambao walikuwa wakigombea eneo la kiwanja ambapo baada ya kugombana wenyewe kwa wenyewe kwa muda mrefu kidogo, hatimaye suala hilo lilifikishwa kwa wazee wa mtaa, ambao baada ya kushauriana, walimtaja mmoja wao kuwa ndio mmiliki halali wa eneo hilo.

Bahati mbaya sana ni kuwa mgogoro huu ulihusisha watu wawili wenye uwezo tofauti kifedha, na bahati mbaya zaidi ni kuwa uamuzi ulipotoka, aliyetajwa kuwa mmiliki halali wa eneo lile, alikuwa ni Yule mwenye uwezo duni kifedha kulinganisha na mwenzake. Sasa hapa shughuli ndio ikaanza upya. Maana licha ya kuelezwa kuwa eneo lile ni lake, jamaa bado aliendelea kulalamika mitaani kuwa mwenzqke anamuonea kwakuwa yeye ana uwezo wa kifedha.

Nilikutana na huyu mlalamikaji siku moja, katika vikao vyetu vile vya jioni, na baada ya utangulizi wa kawaida wa vikao kama vile, akanimwagia mkasa wake na nilikuwa na maswali machache sana ya kumuuliza, nikianza na kama ana waraka wowote ule kuhusu yeye kuwa ndio mmiliki halali wa eneo linalolalamikiwa.

Jibu lake lilikuwa ndio, na nikamuuliza kama ndivyo, kwanini anaendelea kulalamika mitaani tu hachukui eneo lake, ambapo alinijibu kuwa Yule mgombani mwenzie, hataki kuondoa vitu vyake alivyoweka sehemu husika na anaringia fedha zake. Ndipo hapo nilimuuliza kuwa, je, yeye akiwa kama mtu ambaye ameshatajwa kumiliki eneo lile kihalali, alichukua hatua gani kurejesha eneo lake toka kwa mpinzani wake?

Kisa hiki ni kirefu zaidi, kwa wale wanaovielewa vizuri vikao vya jioni, kule mahali kwetu kule, wanaelewa zaidi kile ninachokisema. Lakini mambo ya msingi ninayopenda kuyaangalia ni haya yafuatayo.

Kwanza kabisa, ni kuwa kulikuwa na mgogoro wa wazi wa eneo la kiwanja, pili huyu anayeonekana kuwa muathirika zaidi katika tukio hili, alishaelezwa wazi kuwa eneo lile ni lake na mamlaka husika na la tatu ni changamoto ya kuwa baada ya hapo, ni jukumu la nani kuchukua kilicho chake? Haya ndio ambayo ningependa turejee nayo katika makala yangu ya leo kuhusu kauli ya Malecela, na kwanini nasema hatukumsoma vizuri.

Kwamba ufisadi, ukosefu wa uadilifu na matatizo mengine mengi yamekuwa yakikikumba CCM hivi sasa, hilo ni jambo lililo wazi ambalo limeshajadiliwa kwa kina sana na watu mbalimbali, wakiwemo wana CCM wenyewe ambao wanasubiri tu kulipukiana hivi sasa (hivi hawajalipukiana bado?)

Lakini licha ya matatizo yote hayo, ukweli ni kuwa wanaoitwa mafisadi, wafanyibiashara, viongozi wasio waadilifu na hata mwendawazimu mwingine yeyote Yule, hakuna ambaye ameweza kubadilisha misingi ya Chama cha Mapinduzi. Kwamba ni chama cha Wakulima na Wafanyakazi wa Tanzania. Kwamba ni chama ambacho kimelenga kuzidi kuitambulisha Tanzania, kama taifa lililotukuka kwa amani, mshikamano nk.

Ndio. Matatizo yote yaliyoko ndani ya CCM, likiwemo hili kubwa kabisa la chama kushikiliwa au kuongozwa na viongozi wachafu kimaadili, wasanii wasio maanisha wanachokisema, au wafanyibiashara wanaokitumia kwa ajili ya kujinufaisha, hayamaanishi kuwa misingi ya chama imebadilika. Ila watu wanaopewa dhamana kutuongoza kupitia cha, ndio wamepoteza misingi ya uongozi.

Na mzee Malecela, kutamka kuwa CCM, bado kingali ni chama cha wakulima na wafanyakazi, hajakosea lolote lile, kwani bado miongozo yote ya chama ingali inaonyesha hivyo. Na ingawa ni haki ya kila mtu kumuona kuwa hayuko sahihi kwa msingi ule ule wa tafsiri ya kitu hutokana na mtu anavyokiona kitu husika, lakini binafsi nathubutu kusema kuwa tumetafsiri ndivyo sivyo kauli ile.

Akiwa kama mmoja wa makada maarufu na wenye uwezo mkubwa wa kila kitu ndani ya chama, kiasi cha kufananishwa na tingatinga, mzee Malecela, ni wazi ameona kuwa kuna matatizo ndani ya CCM, lakini bado anatuambia kuwa chama kina wenyewe na wenyewe ni wakulima na wafanyakazi. Kwangu mimi, kauli ile ilimaanisha kuwa ni wajibu wa kila Mtanzania, aliye mkulima na mfanyakazi, kuchukua nafasi yake na kutimiza wajibu wake kukirejesha chama katika misingi yake.

Kauli za visingizio kuwa kuna watu wenye nguvu ndani ya chama, sijui wenye kitu gani, ni kauli za kujidhalilisha ambazo tumekuwa tukiziendekeza sana sisi waswahili, kwa lengo la kutotimiza wajibu wetu, na kasha baadae kuanza kulalamika kuwa tunaonewa na Fulani sijui kwakuwa ana hiki na kile.

Hivi, pesa za mtu zina nguvu kuliko kura zetu? Hivi, tusipompa Fulani kura, atapataje nafasi ya kukitumikia chama kwa manufaa yake? Hivi tukisimama na tukasema kuwa Fulani hatumtaki, atabakia hapo alipo kwa nguvu ya fedha zake kweli? Hivi, hao wanaowaweka hao akina Fulani katika uongozi si ni sisi sisi wakulima na wafanyakazi, vibarua na ambao hivi sasa tunafanywa manamba katika nchi yetu? Kwanini tusikatae?

Inapotokea mtu kakuvua nguo kwasababu ulikuwa unacheza naye mchezo wa kusingiziana, lakini ikathibitika kuwa nguo ile ni yako, unakaa uchi na kulalamikia kuachwa uchi au unachukua nguo yako kwa njia ambayo unajua inawezekana? Ukishaambiwa kitu ni chako, bado unasubiri tena mtu huyo huyo aje akuletee kilicho chako mkononi?

Mzee Malecela, katuambia kuwa chama ni cha wakulima na wafanyakazi. Ni jukumu la wakulima na wafanyakazi kuchukua hatua za kukirejesha chama chao mikononi mwao, badala ya kukubali kununuliwa kwa pombe, kanga, fulana na pilau za msimu, kasha kuanza kuwachambua wale wanaotuambia kuwa kile tulichookiachia ni chetu na kuwalalamikia kuwa wanatudanganya.

Hayati baba wa taifa aliwahi kunukuliwa akisema “inawezekana, timiza wajibu wako”, na bilashaka hata mzee Malecela, anajua kuwa inawezekana kabisa kwa wakulima na wafanyakazi kuchukua chama chao toka mikononi mwa mafisadi, wala rushwa na wasanii wachache ambao wamekaa pale juu kwa ridhaa yao, na akiwa kama muasisi, kiongozi na mtu ambaye angali na nguvu ndani ya chama, anatuambia kuwa hatutakuwa na kosa lolote kuchukua chetu.

Hebu tutafsiri kauli yake in a positive way, kasha tuchukue hatua na tuone kama kweli alikuwa anatupaka mafuta kwa mgongo wa chupa au kutuvika vilemba vya ukoka. Mzee huyu amezungumza, hebu tuzungumze naye lugha moja, tuache kusema sema ovyo.

Wakatabahu……ni mtazamo tu
Share on Google Plus

About Rama Msangi

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni: