side ads

Tuukubali ujinga kwa kisingizio cha Maendeleo?


Naam, hilo ndilo swali ambalo limekuwa likizidi kunijia kichwani kwa kadiri ambavyo nimekuwa nikiendelea kuwa mshabiki na mpenzi wa kazi za wasanii wetu wa maigizo, ambao kila kukicha wamekuwa wakiibuka wapya, kuibua kitu kipya, na kuzidi kutukamata mashabiki kwa kazi zao.

Nikiri tu kuwa, miongoni mwa mambo ambayo yamekuwa na maendeleo ya aina yake hivi sasa katika tasnia ya kisanii humu nchini katika miaka ya hivi karibuni, ni hili la sanaa ya uigizaji. Hakika ni moja kati ya mambo ambayo yakiendelea kwa kasi hii hii, itafikia wakati sekta hii itaitoa nchi yetu kama ambavyo Hollywood ilivyoitoa Marekani, Nollywood na Nigeria, Bollywood katika India. Ndio, sasa ni zamu ya Bongowood bilashaka.

Kwamba wasanii wa sanaa hii, waandishi wa filamu, wazalishaji na wadau wengine wa mekuwa wakiibuka kila kukicha, wakiwa na kitu kipya, hadithi mpya, ikiwa katika ubora kuliko wa ile ya jana, hii ni ishara ya wazi kuwa sekta hii imekubalika miongoni mwetu na wasanii nao wameridhishwa na kiwango wanachoungwa mkono na jamii inayowazunguka.

Hata hivyo, kwa kadiri ambavyo siku zinazidi kwenda, sanaa nayo ikzidi kukua kwa kasi ya aina yake, ndivyo ambavyo kumezidi kuwa na dalili za wazi za sanaa hii ya maigizo kujionyesha kuwa huenda isiwe sanaa ambayo itakuwa na manufaa makubwa kwa jamii ya Kitanzania, hili likitokana na ukweli kuwa, kumekuwa na dalili za wazi wazi za uvamizi unaofanywa na watu ambao hawaelewi kanuni na misingi ya uigizaji.

Wimbi la kuibuka kwa watu maarufu kuamua kujiingiza katika tasnia hii, si jambo ambalo ni la kulifurahia sana, licha ya wahusika, na hapa nikimaanisha kuwa wale ambao wameshakuwa wakongwe, kulielewa hili, wamekuwa wakizidi kuliacha lizidi kukua siku hadi siku.

Si hali nzuri kwani uigizaji sio sehemu ya kutangazia umaarufu wa mtu, hili likimaanisha kuwa tasnia hii kuwakubali watu wa aina hiyo, ni kuanza kuiua waziwazi fursa hii muhimu na ambayo imeshaanza kukubalika kwa jamii.

Ni hivi, kawaida mtu ambaye hawezi kufanya kitu Fulani, lakini ambaye ameweza kuingia mahali hapo, hujitahidi kutumia kila alicho nacho kuona kuwa anaonekana mahali hapo, bila kujali kuwa njia anayoitumia ni muafaka au laa. Na inapotokea kuwa waliomkaribisha ama kumshirikisha sio watu wenye sauti za kuweza kumkemea, basi tatizo huwa kubwa zaidi, maana humuacha tu afanye madudu yake ilimradi siku ipite.

Nitatolea mfano wa wimbi la wanamuziki, wanamitindo na walimbwende kuvamia fani ya uigizaji hapa nchini. Hili limeshakuwa jambo la kawaida sana hivi sasa. Sihitaji kuwataja majina watu wa namna hii, maana wanajijua. Ninachotaka kugusia hapa ni je, wamekuwa na mchango gani hasa katika kukuza utamaduni wetu wa kitanzania kupitia filamu?

Uvaaji wa hovyo hovyo, ambao tulio wazalendo hatuhasita au kukosea kuuita wa nusu au robo tatu uchi, limekuwa ni jambo la kawaida katika filamu nyingi zinazotoka sasa, mtindo huu ukiwa umeasisiwa na watu wa fani ya urembo na ulimbwende walioamua kujiingiza katika fani hii. Je, hili ni jambo la kujivunia kweli?

Sikatai kuwa, filamu kama moja ya mambo ambayo hugusia kwa karibu sana mambo yenye kuendelea katika jamii, mara nyingi huakisi yale yanayotokea katika jamii husika, na kwamba hili la uvaaji wa nusu au robo tatu uchi ni miongoni mwa mambo ambayo yamekuwa yakizidi kuzoelekeka nchini hivi sasa. Lakini je, wasanii nao wanatakiwa kuendelea kutetea na kuutangaza utaratibu huu kama wafanyavyo eti kwakuwa tu unatokea miongoni mwetu?

Kazi ya sanaa kwa kawaida ni pamoja na kuifundisha jamii. Je, ni kipi ambacho wasanii wetu na niwe wazi tu, dada zetu wanachotaka tujifunze kupitia uvaaji wao kwenye filamu mbalimbali wanazocheza?

Ni kweli kuwa sanaa hii ya maigizo imekuwa inashika kasi ya ajabu sana na ni wazi kuwa imetoa ajira za kutosha tu kwa vijana wengi wa kitanzania, huku pia ikiwa sehemu ya mambo yenye kuchangia katika pato la taifa. Na ni wazi kuwa kwa kasi hii tutafikia mahali ambapo sekta hii itakuwa moja ya sekta zenye kutoa asilimia kubwa ya ajira kwa vijana wa kitanzania na kuchangia asilimia kubwa katika pato la taifa.

Lakini je, tunatakiwa kuufumbia macho ujinga, upotoshwaji wa maadili, uvaaji wa hovyo na tabia zingingine zisizo za Kitanzania, eti kwasababu tu ya maendeleo? Tuukubali ujinga kwa kisingizio cha maendeleo? Tutafakari na kuchambua pamoja
Share on Google Plus

About Rama Msangi

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

2 maoni:

Bwaya said...

Nimepita kutia saini katika kitabu cha wageni. Nimesoma na kujifunza mengi. Kazi nzuri mkubwa.

Anonymous said...

comment012, buy adobe photoshop oem, vzxzw4, cheap adobe creative suite, xmaiu9, cheap adobe photoshop lightroom, lclaw1, cheap office 2007 enterprise, eifgn1, buy corel painter 11, cgnow1