side ads

TUICO & FIBUCA na sera mpya ya utengano ni nguvu

MAMBO yanayoendelea hapa nchini hivi sasa, yananikumbusha kipindi kile huu muziki wa kisasa unaojulikana zaidi kwa jina la ‘Bongo Fleva’, ulipokuwa unachipukia, ambapo msanii aliweza kukurupuka asubuhi kuingia studio kurekosi singe yake kutokana na mistari aliyoitunga baada ya yaliyojiri baina yake na kiburudisho chake usiku wa kuamkia siku hiyo.

Ukiachilia mbali single ya kitaifa inayoendelea kutesa sana kimauzo, inayokwenda kwa jina la Dowans, na ile ya kimataifa ya ‘kupinduliwa’ kwa raisi wa Madagascar, zenye kuhusisha maslahi ya kisiasa zaidi, ambazo zilitamba sana wiki jana na zinazoendelea kutamba hata wiki hili, single nyingine ambayo ilizinduliwa mwanzoni mwa wiki hili, ni ile inayokwenda kwa jina la FIBUCA, yenye kuhusisha wafanyakazi nchini Tanzania.

"Financial, Industrial, Banking, Utilities, Commercial, Agricultural and Allied Workers Union" (FIBUCA), hiki ni chama kipya cha wafanyakazi wa taasisi za fedha viwanda biashara na kilimo, ambacho kilitambulishwa rasmi mwishoni mwa wiki jana, kikitokana na kumeguka kwa TUICO, chama ambacho awali kilikuwa kikimeza taasisi zote hizo.

Kwa baadhi yetu ambao tulibahatika kukutana na taarifa za utambulisho au uzinduzi wa chama hiki, bila shaka tulisikia mengi yaliyozungumzwa na viongozi mbalimbali wa chama hiki, akiwemo raisi wake Bw. Mussa Nyong’onyo, ambaye hapo kabla alikuwa ni mwenyekiti wa TUICO-Temeke. Miongoni mwao zikiwemo sijui kuwa naweza kuzipa jina lipi kati ya tuhuma, lawama, madai, kejeli, vijembe au manung’uniko, aliyoyatoa dhidi ya TUICO, na kuyaita kama sababu za msingi za kuanzishwa kwa FIBUCA.

Kimsingi, kuanzishwa kwa chama hiki, bilashaka ni utekelezaji wa matamko kadhaa ya haki za wafanyakazi, ambao kama sehemu muhimu ya jamii, wana uhuru wa kuanzisha na kuendesha vyama, kwa minajili ya kulinda na kutetea maslahi yao sehemu za kazini. Lakini je, uanzishwaji wa chama hiki, ni muarobaini wa kadhia mbalimbali wanazokumbana nazo asilimia kubwa ya hawa waliopachikwa jina la wafanyakazi hapa nchini, lakini wakiwa hawajaliwi kulingana na mchango wao kwa taifa hili?

Malumbano ndani ya TUICO, moja kati ya vyama vikongwe vya wafanyakazi hapa nchini, na ambacho kimekuwa na nguvu kubwa sana kiushawishi na kiutekelezaji, ni jambo ambalo licha ya kuonekana kuwa la siku za karibuni, lilikuwa la muda mrefu sana. Na ninathubutu kusema kuwa, ni mwendawazimu tu ambaye anaweza kukataa kuwa malumbano au mgogoro huo haukuwa ukihusisha maslahi binafsi zaidi kuliko maslahi ya wafanyakazi.

Na licha ya kuwa jitihada kadhaa kubwa zilizofanywa, haiyumkiniki ndio maana muafaka ulishindwa kufikiwa ili kurekebisha hali hiyo, kwasababu ushiriki wa wadau katika kutatua tatizo hili, ulizidiwa na utashi wa kimaslahi binafsi zaidi kuliko maslahi ya wanachama wa chama hicho.

Na ndipo hapo ilipofikia hatua ya kundi Fulani kuamua kujiondoa na kuanzisha chama kingine, kwa kufuata mkondo ule ule wa maisha ya kisasa ya Watanzania, wafanyakazi wakiwemo, na hapa nazungumzia mkondo wa kisiasa.

Ninasema kuwa hatua hii ya kuanzishwa kwa chama kipya, ni hatua ambayo ilikuwa na mizizi ya kisiasa iliyochanganyika na mbolea ya maslahi binafsi zaidi kwasababu, kwa bahati mbaya sana, mimi si mmoja kati ya wale wenye kuamini kuwa kukimbia matatizo ndio suluhisho la matatizo hayo. Na ikiwa kweli kulikuwa na tatizo ndani ya TUICO, basi kuanzishwa kwa FIBUCA, ni sawa kabisa na kulikimbia tatizo badala ya kukabiliana nalo.

Ni bahati mbaya sana kuwa hatua hii pia ilikuja katika kipindi ambacho Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda, alikuwa akikutana na viongozi wa vyama mbalimbali vya wafanyakazi, ambapo moja ya mambo aliyoyazungumzia katika mikutano yake hiyo iliyohusisha pia chama cha TUICO, lilikuwa ni la kuhimiza mshikamano baina ya vyama vya wafanyakazi.

Mshikamano kwa maana ya kuwepo kwa muungano ambao utawezesha kuwa na vyama vichache sana lakini ambavyo vitakuwa na nguvu kubwa linapokuja suala la kujadili maslahi ya wafanyakazi, kuliko kuwa na utitiri wa vyama lakini ambavyo havitakuwa na nguvu kwakuwa kila kimoja kitakuwa na sauti yake, jambo ambalo litakuwa na faida kwa waajiri zaidi kuliko waajiriwa ambao ndio walengwa wa Vyama vya wafanyakazi.

Ukijaribu kuzama kwa undani kidogo katika masuala haya, utabaini kuwa miongoni mwa mambo ambayo yameendelea kuwagharimu wafanyakazi ni pamoja na kulegalega kwa vyama vyao, vingi kati yao ikitokana na utendaji wa kulegalega wa baadhi ya viongozi wake. Lakini ukuzama zaidi utabaini kuwa tatizo pia haliko kwa viongozi hao, bali mfumo mbovu wa uongozi ambao vyama hivyo vinakuwa vimejiwekea, ambao ndio huruhusu au kutoa mianya kwa baadhi ya watendaji kuwa wabovu na walafi wa mali za vyama.

Haiyumkini ndio maana basi, lilipoibuka sakata la tuhuma zilizokuwa zikiwakabili baadhi ya viongpozi wa TUCTA, hadi kuamuliwa kusimamishwa ili kuruhusu uchunguzi kufanyika, ndio maana yaliibuka haya yote ya sasa kwakuwa waliochukuliwa hatua waliona wazi kuwa wameonewa kwakuwa sera na taratibu za muundo wa vyama vyao, zilikuwa upande wao.

Nilicheka sana siku niliposoma kuwa eti kuna tawi moja linashinikiza kujiuzulu kwa katibu mkuu wa TUICO, Bonface Nkakatisi, kwa madai ya kuwa ni kipofu. Nilicheka kwasababu, miezi kadhaa iliyopita wakati anasimam a kujadili suala mgogoro wa wafanyakazi wa NMB, kila mfanyakazi alikuwa akimtolea macho yeye, na kumsikiliza yeye. Je, upofu wa Nkakatisi umekuja kwa ghafla kiasi hiki baada tu ya kusimamishwa kujadiliwa kwa tuhuma za ufisadi ndani ya TUCTA?

Na nikavinjika mbavu zaidi pale niliposikia kuwa, NBC, wamemtaka ajiuzulu kwasababu walienda ofisini kwake na akawakimbia. Sijui kiwango cha busara cha wajumbe wa TUICO kutoka NBC, kuwa ni cha kiwango gani, lakini kwa kauli na tamko lile, ni wazi kuwa kilijipembua kuwa ni cha chini sana.

Ingawa sitopenda kuzama sana katika hoja hii, lakini swali moja tu ambalo ningependa kuwauliza wana TUICO kutoka NBC, ni je, ikiwa mimi mteja nimezoea kuhudumiwa na mhudumu Fulani katika moja ya benki zao, na siku moja nikafika naye akatoka asinihudunie, je, kitendo hicho cha siku moja, kinatosha mimi kwenda kwa meneja na kuomba mfanyakazi huyo afukuzwe kazi kwani hafai na nikatishia kufunga akaunti yangu ikiwa hatofukuzwa?

Haidhuru, kwenye mgogoro wowote ule, na hasa wenye kuhusisha maslahi binafsi zaidi kama nilivyoainisha hapo awali, ni jambo la kawaida sana kwa silaha zenye kutumika huko kwa kawaida hazijali kiwango cha busara au uwezo wa kufikiri, bali huzingatia kiwango chake cha uteketezaji wa mpinzani, na ndio maana mashambulizi huweza pia kuwa yenye kumlenga mtu kwa mambo yake binafsi zaidi kuliko kingine chochote kile.

Nimekuwa nikifuatilia kwa ukaribu sana malumbano na mgogoro uliokuwa na unaoendelea TUICO, kutokana na sababu mbalimbali na jambo ambalo nimeweza kulibaini ni kuwa tatizo halikuwa TUICO kama chama, bali baadhi ya watu ambao maslahi yao ni jambo la muhimu zaidi kuliko kitu kingine. Washibe wao, wafanyakazi waendelee kuteseka. Waendelee wao kufaidi hela za posho za vikao vya majadiliano (kama zipo kweli), huku wafanyakazi wakiendelea kuotea jua wakitumaini kivuli kuja wakati wowote.

Tatizo ni mifumo, sera na taratibu ambazo zimeandaliwa bila kuzingatia masuala ya muhimu ambayo yatavifanya vyama hivyo kustawi, bali kudorora, na hivyo kudhoofisha wafanyakazi huku waajiri wakiendelea kuhenyeka kwa kujipepelea miili yao kutokana na kunona kwa afya zao.

Hebu tujiulize kwa haraka haraka, raisi wa FIBUCA, akiwa mwenyekiti wa TUICO-Temeke, kiongozi wa juu kabisa tena toka eneo lenye nguvu sana na ambalo likikohoa lazima kishindo kisikike, alipoona kuwa kuna tatizo ndani ya chama hicho, alifanya nini la maana kuhakikisha mgogoro huo unaondoka haraka ili chama kibakie na maslahi ya kutetea wafanyakazi badala ya malumbano?

Anaweza kutueleza leo hii kuwa nini chanzo cha mgogoro huo unaokisambaratisha chama hivi sasa, nay eye alifanya nini kwa mujibu wa katiba ya TUICO, kuhakikisha kuwa hali haifikii hapa ilipo hivi sasa? Au chama hakina katiba ambayo inaainisha wazi namna ya kushughulikia matatizo ndani ya chama? Na kama chama kina katiba yenye kuelezea namna ya kutatua migogoro inapoibuka ndani ya chama alifanya nini na nini kuhusiana na vipengele hivyo?

Na ikiwa katiba haikuwa na kipengele kama hicho, haoni kuwa ulikuwa upungufu wao mkubwa ambao waliuandaa kwa lengo la kila mmoja kulinda maslahi yake zaidi kuliko ya chama na wafanyakazi wenye kukitegemea chama hicho?

Maswali haya pia, ningelipenda sana wayajibu watendaji wengine waliopachikwa majina ya ‘wa muda mfupi’, ambao naamini kila mmoja kwa namna moja ama nyingine alikuwa na wadhifa au nafasi Fulani ndani ya TUICO, kalba ya kujiengua na kuanzisha FIBUCA. Ndio, walifanya nini hasa walikotoka zaidi ya kuwa walitengeneza mazingira ya kuzuka mgogoro na hatimaye wao wakaukimbia badala ya kuukabili?

Na ikiwa walishindwa kuweka kanuni za wazi za kiutendaji zitakazozuia kuibuka kwa malumbano na migogoro ndani ya TUICO, au kuweka mazingira na kanuni madhubuti ambazo zitawezesha utatuzi wa migogoro kwa nia sahihi na za wazi huko ndani ya TUICO, tuwaamini vipi kuwa hawatafanya hayahaya ndani ya chama kipya? Tuwaamini vipi kuwa hawajaanzisha chama hiki kwa lengo lile lile alilokemea waziri mkuu, la kuwa dhoofisha nguvu za wafanyakazi kwa kuanzisha utitiri wa vyama ambavyo vitakuwa vikilinda maslahi ya viongozi wa vyama hivyo badala ya ya wafanyakazi?

Ni wazi kuwa sehemu kubwa wanaohusika na mada hii hawasomi blogi, lakini naamini kuwa, taarifa zitawafikia kuwa kuna jambo ambalo wanatakiwa kulizungumzia mahali, na nitapenda ushiriki wao katika kujadiliana hili, kupitia hapa hapa Jukwaani.

Ni mtazamo tu… nikiamini kuwa majadiliano ndio niia muafaka ya kuelekea maendeleo endelevu.
Share on Google Plus

About Rama Msangi

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni: