side ads

TAIFA LETU LINAANGAMIA.... mustakabali wa nchi umewekwa rehani

“Mimi nafikiri swali hili angeulizwa Rostam. Kwamba yeye anapotuma vijana kuanza kutuchafua wenzake, yeye anafikiriaje? Nafikiri angeanza yeye, maana mimi naongea very politely hapa, lakini kuna siku tutafyatuka. Yaani tusiheshimiane kabisa” ..........Dk. Harrison Mwakyembe, mbunge wa Kyela (CCM), akijibu mkombora aliyotupiwa kuhusu mradi “wake” wa kufua umeme wa upepo.

Naam. Nimebahatika kuusikiliza, kuusoma na hata kuufuatilia kupitia wachambuzi mbalimbali, utetezi wa Dk. Mwakyembe, dhidi ya kombora alilotupiwa, na nimeridhika kabisa kuwa, kauli ya mbunge wa kyela kupitia CCM, ina maana zaidi ya kujitetea au kujihami kutokana na kombora alilotupiwa kuhusu mgongano wa kimaslahi baina ya ubunge wake, ujumbe wake kwenye kamati za Bunge na umiliki wa mradi wa kufua umeme kwa kutumia upepo.

Ndio, kama kwa hali ilivyo sasa, mwanasheria na mwandishi huyu anatuambia kuwa ipo siku watafyatukana ipo siku wataacha kuheshimiana! Ni wazi kabisa kuwa, kuna zaidi ya kujitetea katika matamshi yale.

Kwa namna yoyote ile, licha ya jitihada zinazowezatumika katika kulipinga hili, ukweli hauwezifichika kwamba, ndani ya Chama cha Mapinduzi. Baada ya kushika hatamu za uongozi wa nchi hii kwa zaidi ya robo karne sasa, chama hiki hivi sasa kimepoteza dirana uelekeo, maadili, heshima, busara na hata uaminifu wake kwa mamilioni ya Watanzania ambao wamekuwa wakikipa dhamna ya uongozi toka kianzishwe.

Itoshe tu kusema kuwa, kama ni mtumbwi, basi chama hiki kimepoteza kasia, na sasa marejeo yake ufukweni, yangeweza angalau kutegemea upepo, lakini kwa bahati mbaya zaidi ni kuwa, jahazi hili halina hata tanga, ambalo linaweza kulisaidia liwezeshwe na upepo kufika huko pwani, na kwa kadiri waliomo chomboni wanavyozidi kuchojoa nguo zao, waungeunge na kuzifanya tanga la kukinga upepo, ndivyo kinavyozidi kupoteza uelekeo maana upepo wenyewe unazidi kugeuka kuwa wa maruhani zaidi.

Katika miaka ya hivi karibuni and to be specific, katika zama hizi za awamu ya nne ya utawala wa nchi, mambo ambayo yamekuwa yakiendelea ndani ya chama hiki, hakika haitoshi kuyaita ya ajabu wala ya kijinga, maana ni zaidi ya hapo. Binafsi nashindwa kupata neon muafaka la kuyaita mambo ambayo yamekuwa yakiendelea ndani ya CCM, katika miaka ya hivi karibuni, maana kizunguzungu si kizunguzungu, kichefuchefu si kichefuchefu… ilimradi shaghalabaghala tu.

Siasa za majungu, umbeya, uzushi, chuki, visasi, na asilimia kubwa ya viongozi wenye kujali maslahi ya matumbo yao zaidi, ndio mambo ambayo yamekitawala chama hiki hivi sasa, na haiyumkiniki ndio maana hata wale wachache wenye kuonekana kama wangeweza kunusuru jahazi, juhudi zao ni kama za kutaka kukausha bahari kwa kutumia bilauri, jambo ambalo ni sawa na ndoto za abunuwasi.

Ndio, katika zama hizi ambazo nchi imekuwa katika matatizo lukuki, ndio kipindi hiki hiki ambacho tumekuwa tukizidi kushuhudia wimbi kubwa la viongozi mbalimbali wa chama (ambao pia asilimia kubwa kama si wote, ndio viongozi wa kiserikali pia), wakikiuka maadili ya kila kitu katika taifa hili.

Ni katika kipindi hiki ambapo tunashuhudia Bunge likiendeshwa magazetini, luningani na redioni, huku kila mmoja akijitwalia madaraka ya kuwa msemaji wa Bunge, popote na wakati wowote anapojisikia, kana kwamba chombo hiki kimekuwa mtumba wa sagulasagula pale Kariakoo, ambapo kila mmoja anaweza kufika na akaushikashika bila kujali usafi wa mikono yake, na muuzaji akabakia kumkenulia meno.

Ni katika kipindi hikihiki ambapo tunashuhudia viongozi na hata baadhi wakiwa wapigadebe tu wa CCM, kila mmoja kwa wakati wake, akikurupuka na kusimama jukwaani mahali Fulani na kasha akaisemea serikali kuhusu jambo Fulani hili au lile. Ni katika kipindi hiki hiki tunashuhudia vitosho vya waziwazi baina ya viongozi wa kada mbalimbali, na mashindano ya kila mmoja kutaka kumpiku mwenzake kimadaraka nk.

Lakini kibaya zaidi, ni katika kipindi hiki hiki ambapo tunashuhudia ukimya wa hali ya juu kwa viongozi ambao walitakiwa kuonyesha (japo kwa kutamka tu), kuwa hawaridhishwi na hali hii, lakini hatuwasikii. Sijamsikia Spika wa Bunge la Tanzania akikemea tabia ya wabunge wengi kutumia muda mwingi kujadili masuala ya ndani ya Bunge, wakiwa mitaani na vijiweni. Na bilashaka huenda kimya chahe kinawafanya wahusika nao kuona ni jambo la kawaida kabisa kuendelea kuchafua hadhi ya chombo hiki kitukufu.

Sijamsikia Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Mrisho Kikwete, akisimama hadharani kukemea tabia ya wajumbe wa halmashauri kuu, kamati kuu na hata mkutano mkuu wa chama, kuwataka waache tabia hiyo au hata kuwachukulia hatua, kwakuwa chama hicho kina taratibu na kanuni zake zinazokiongoza na sio kuzungumza kupitia vyombo vya habari.

Sijamsikia mheshimiwa Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mheshimiwa Jakaya Kikwete, pia kusimama na kukemea tabia ya baadhi ya mawaziri wake, kutumia vyombo vya habari katika kuhanikiza masuala ya kitaifa ambayo yamekuwa yakiliweka taifa katika hali tete. Na bila shaka ndio maana Mhheshimiwa Membe, aliwahi kutoa tamko la kuwahakikishia Watanzania kuwa mchakato wa kujiunga na OIC, ungekamilika ndani ya wiki moja, lakini yeye Raisi baadae akaja kutamka kuwa ndio kwanza kamati imeundwa kulishughulikia.

Swali unaloweza kujiuliza hapa ni, Je, woga huu wa wanaotakiwa kuchukua hatua unatokea wapi, hasa kwa kuzingatia kuwa kila mmoja aliingia madarakani kwa mbwembwe ambazo ziliwapa watanzania matumaini ya kuwa mwisho wa viongozi wasio waadilifu ndio umewadia? Je, jeuri ya hawa wanaoendelea kuvunja maadili ya uongozi kiasi cha kuiweka rehani hali ya utulivu (japo wa kinadharia), tulionao nchini inatoka wapi?

Bilashaka mwanzo wa visa vyote hivi, ulikuwa wakati ule wa kampeni za kuwania nafasi ya kugombea kiti cha uraisi kupitia CCM. Ni katika kipindi kile ambapo siasa za kuchafuana na za majungu ziliibuka kwa kasi ya ajabu sana. Lakini kwakuwa wengi wa waliotakiwa kuchukua hatua kuzuia kirisi kile kuendelea walikuwa wako katika harakati za kuwania ulaji, waliliacha kama lilivyo. Baadhi kwasababu lilikuwa likiwasaidia, na baadhi kwasababu waliona halitawaathiri.

Matokeo yake ilikuwa kuibuka kwa makundi ndani ya chama, makundi ambayo ili kuhakikisha ushindi, ilikuwa shurti yajue undani wa mtu wanayempa sapoti, ili wajue namna ya kufukia maovu yake wakati wakimnadi, na vile vile wajue maovu ya mpinzani wao ili waweze kuyatumia kikamilifu kummaliza. Na mbinu hii ilifanikiwa kwa kiasi kikubwa sana. Ni wachache sana na nadhani hakuna aliyeshinda kupitia CCM, mwaka ule anayeweza kusimama hadharani na kukiri kuwa nyuma ya ushindi wake hakukuwa na makundi au siasa za kuchafuana.

Hata raisi mwenyewe baada ya ushindi, alitangaza hadharani kuwashukuru wana-mtandao, ambao walifanikisha ushundi wake huo. Na hapana shaka kuwa, ule ndio ulikuwa mwanzo wa Tanzania kuwa msambweni. Kwasababu baada ya pale, ndipo makundi yakajionyesha waziwazi licha ya rai ya kutaka yavunjike ili kazi ya ujenzi wa taifa iendelee kwa pamoja, rai ambayo aliitoa mheshimiwa raisi.

Majeruhi waliotokana na kushundwa wakaanza rasmi kusaka wachawi wao, huku walioibuka washindi nao wakizidi kugawanyika kutokana na baadhi yao kujeruhiwa kwa kukosa nafasi za ‘fadhila ya kufanikisha ushindi’. Haya hayakuchukuliwa hatua wakati huo, kwakuwa kila mmoja alipuuzia kutokana na sababu anazozijua mwenyewe, ingawa kubwa kabisa ilikuwa imeegemea katika ile dhana ya ‘asiye na dhambi awe wa kwanza kurusha jiwe’

Ndio, ni nani ambaye angeweza kuthubutu kurusha jiwe la kukemea madudu yale wakati yanaanza wakati wenye kustahili kukemea ndio kwanza kila mmoja alikuwa anaanza kuonja utamu wa joto la kiti cha kuzunguka katika ofisi yenye kiyoyozi? Angemgusaje au kumnyooshea vipi kidole mwingine wakati anajua wazi ni mwelewa wa madhambi yake yote aliyowahi kuyatenda? Sasa je, amguse ili amulipue naye aukose uhondo wa kutembelea gari la kifahari na marupurupu ambayo ndio kwanza alikuwa akianza kuyaonja! Hapana, haikuwezekana.

Waliokuwa wakitizama mbele zaidi, walijua wazi kuwa hali hii ni hatari kwa usalama wa taifa letu, walijaribu kukemea hali hii, lakini nani ambaye angewasikia wakati wahusika walikuwa tayari wameshajifungua katika ofisi ambazo ni sound proof? Matokeo yake ni kwamba, kwa sasa hivi, inamhitaji mtu kuwa na akili zisizofanya kazi kawaida kutetea mustakabali wa taifa letu kuwa uko katika njia sahihi. Maana ukweli ni kuwa tuko msambweni tayari.

Hivi sasa asilimia kubwa ya wabunge hutumia muda wao wan je ya vikao kujadili makombora wanayorushiana, kuzushiana kashfa mbalimbali na kukejeliana kwa kila namna badala ya kuwajibika kwa wananchi wao. Na wanaporejea Bungeni wakati wa vikao, hutumia muda huo kujadili miradi ambayo ilishajulikana wazi kuwa inalitia taifa hasara, wizi wa fedha za serikali na mambo ya namna hiyo. Mwananchi aliyewachagua, hana nafasi tena.

Serikalini nako, asilimia kubwa ya viongozi wanatumia muda wao mwingi kuweka mambo yao sawa ili matumbo yao nay a watoto wao yazidi kujaa na kuwawezesha kuhudhuria misalani. Wajibu wao kwa wananchi wanaowaongoza au kuwatumikia, umeendelea kuwa ule wa kutoa matamko ya hapa na pale wakiwa ndani ya suti zao za gharama.

Uchumi wan chi umedorora, hali za watanzania kila kukicha ni afadhali ya jana, kila wanalojaribu kulifanya kujikwamua, limekuwa halina tija, maana hawapati misaada yoyote ya kivitendo, zaidi ya ile ya kisiasa na ahadi hewa ambazo utekelezaji wake nadhani unasubiri kampeni zianze tena.

Yote haya kutokana na viongozi wetu wa kisiasa na wa kiserikali kupoteza uelekeo, kukosa maadili ya kiuongozi, kukosa heshima kwa waliowachagua na kuwapa dhamana ya kuwaongoza. Ndipo hapa tunapoanza kujiuliza, hivi CCM, imekumbwa na nini hadi viongozi wake kuwa wakurushiana makombora magazetini? Ilishavunja ule utaratibu wa kuitana vikao vya ndani kujadili dukuduku zao za kibinafsi na kasha wanapokuwa nje ya vikao kuzungumzia mikakati ya kulijenga Taifa?

Serikali yetu imekumbwa na ugonjwa wa namna gani hasa? Ambapo kila kiongozi anaweza kukurupuka na kusema lake magazetini bila kujali kuwa ana wakubwa zake, watendaji wenzake na washauri wake na ambao anatakiwa kushirikiana nao katika kujadili jambo Fulani kabla ya kulitolea maamuzi ya kimsingi yenye kujenga Taifa?

Kwa namna yoyote ile, maswali ni mengi sana kuliko majibu yake. Kwa namna yoyote ile tayari hali ya nchi ni mbaya zaidi ya maelezo, kiuchumi, kimaadili, kiheshima na kwa kila kitu. Na ikiwa katika muktadha huu bado DK. Mwakyembe, anatuambia kuwa ipo siku watafyatukiana na wasiheshimiane, maana yake ni kuwa ipo siku nchi hii itaingia katika mgogoro ambao hautamithilika na athari zake zitakuwa za kihistoria.

Mungu ibariki Tanzania.
Share on Google Plus

About Rama Msangi

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

1 maoni:

Yasinta Ngonyani said...

umefanya kazi nzuri sana nami nasema MUNGU IBARIKI TANZANIA YETU.