side ads

Eti umechelewa! Ni nani kayawahi maisha?

Miongoni mwa mambo ambayo yamekuwa yakitutatiza wanadamu, wake kwa waume, vijana kwa wazee, watoto kwa watu wazima, ni pamoja na kutokufikiwa kwa malengo, ndoto, mipango au matarajio yetu.

Tupo ambao tulikuwa na ndoto za kuwa watawala wa dunia, tupo ambao tuliwaza kumiliki mali zote za dunia, tupo ambao tuliwaza kuwa na wake wazuri, tupo ambao tuliwaza kuwa wachungaji au masheikh na mambo mengine mengi, lakini leo hii hatuko mahali hapo tulipokuwa tunapawaza au kupaota.

Haya ni baadhi tu ya mambo ambayo naamini ni machache sana miongoni mwa mengi ambayo wanadamu kila mmoja amekuwa akiyawaza au kuyaota kichwani mwake na yasitokee, na kutusababishia maumivu mengi ndani ya mioyo yetu. Tupo ambao tulilia au tunalia sana, wapo waliofikia hatua ya kujiua nakadhalika. Lakini je, tuliweza kufikia suluhisho kutokana na namna tulivyopokea matokeo hayo?

Ni wazi kabisa kuwa ni vigumu sana kwa mwanadamu kutokukumbwa na hali Fulani pindi kile alichokuwa akikiwaza, kukiota, kukitaraji au kukitegemea, kinapotokea ndivyo sivyo. Lakini ni mara ngapi basi tuliwahi kujiuliza kuwa hali ingekuwaje kama kila mwanadamu akitaka kulia humu duniani? Tumewahi kujiuliza kuwa ingekuwaje ikiwa kila mwanadamu hapa duniani atakuwa na mawazo au atathubutu kujinyonga?

Ni wazi kabisa kuwa huenda dunia isingekuwa na watu hivi sasa, kwakuwa ukweli uliowazi ni kuwa hakuna mwanadamu ambaye aliwahi kufanya kila jambo lake na likaleta matokeo kama alivyokuwa amefikiria au kupanga. Ni wazi kabisa kuwa dunia ingekumbwa na mafuriko yatokanayo na machozi, kama kila mtu angeamua kulia, kwani ukweli ni kuwa hakuna mwanadamu ambaye hajawahi kuanguka katika maisha yake.

Katika muktadha huu basi, ndipo hapa tunapojikuta mahali ambako tunatakiwa kukaa na kutafakari kwa kina nini hasa cha kufanya pindi tunapokumbwa na hali ya kutokufikiwa kwa ndoto au matarajio yetu.

Ni wazi kabisa kuwa zipo namna nyingi sana ambazo tunaweza kufanya kuweza kukabiliana na hali za namna hiyo, lakini leo kwa uchache sana nimeona nizungumzie njia nne tu, zinazoweza kukufanya ukawa na amani pindi unapokuwa unakabiliwa na shinikizo la kufeli kimaisha.

> JIJAZE FIKRA CHANYA.
Wataalamu wa masuala ya saikolojia wanatuambia kuwa, kila mwanadamu ni vile anavyojiwazia yeye. Ndio. Ikiwa unajiwazia kwa mtazamo chanya basi ni wazi kuwa utakuwa mtu chanya, na ikiwa unajiwazia kwa mtazamo hasi, basi ni wazi kuwa utakuwa hivyo hivyo.

Ingawa imeshazoelekeka kwamba mtu unapokumbwa na janga au tatizo Fulani, suluhisho ni kulia sana na wengine kufikiri au kufikia hatua ya kujitoa uhai, ukweli ni kwamba kuna mambo ambayo unaweza kuyafanya na ukawa umejitendea haki zaidi kwa kuyafanya kabla ya kuwaza hayo tuliyoyazoea.

Miongoni mwa mambo ambayo unaweza kuyafanya na yakakupunguzia mzigo wa shinikizo la kufeli ni pamoja na kujiuliza maswali kama vile “Je, mimi ndio mtu wa kwanza kutokewa na jambo hili hapa duniani? Je, mimi ndio nitakuwa wa mwisho kukumbwa na kitu hiki?”

Ni wazi kuwa majibu yake yatakuwa hapana. Kama ni hivyo basi, kwanini ufikie hatua ya kujitoa uhai wako wakati wewe si wa kwanza kuwa dunia itakutizama kama mtu uliyeandika historia ya kuwa wa kwanza kutokewa na jambo hilo? Au kana kwamba utakuwa wa mwisho kwahiyo dunia itakutizama kama mtu aliyeweka historia ya kufunga ukurasa wa kutokewa na matukio Fulani?

Tizama kulia kwako na kushoto kwako. Tizama nyuma yako na mbele yako, uone ni wangapi ambao wamekutangulia kukumbwa na hali hiyo na wangali wanavuta pumzi, na wangapi ambao wako katika uelekeo wa kukumbwa na jambo kama hilo na wala hawana mawazo ya kujinyima kuishi. Kasha vuta pumzi ndefu na umwambie Mungu, “Nakushukuru kwa kila kitu, kwani maisha yangu ni kusudio lako maalum”

> ONYESHA JITIHADA.
Wengi wetu tumeshuhudia au kukumbana na hali ya kutofikia malengo yetu Fulani Fulani kiasi cha kukata tama kabisa, jambo ambalo ni bay asana katika maisha yetu. Kukata tama wewe binafsi ni dalili ya kuwaambia watu kuwa mie sihitaji msaada wenu, niacheni kama nilivyo. Na kweli inapotokea hivyo, basi kila mtu hukuacha wewe kivyakovyako, maana unakuwa husaidiki.

Kuanguka ni sehemu ya maisha, tena sehemu muhimu sana ya maisha. Kwasababu bila kuanguka mwanadamu huwezi kuwa na nguvu za kujifunza kuwa makini zaidi. Hivyo basi, baada ya kukubali kuwa kuanguka si jambo la ajabu, jitahidi kujikusanya ili unyanyuke. Na inapotokea mtu akakuona umenyanyuka unajikung’uta vumbi, huenda akakusaidia maji ili uoge kabisa. Yupo ambaye atakupa pole, yupo ambaye atakushauri uende hospitali kuangalia kama umeumia au laa nk.

Lakini wote hawa watafanya hivyo, ikiwa wamekukuta unajitahidi kunyanyuka au kujikung’uta vumbi. Hakuna atakayekukuta umelala chini unapiga kelele za kuomba msaada au umekaa kimya ukitaraji wakunyanyue, na akafanya hivyo, kwasababu wote watakuchukulia kama mtu uliyelewa na wakakuacha kwa raha zako.

> YAKATAE MATATIZO YAKO, ZIKUBALI CHANGAMOTO
Mwanazuoni mmoja aliwahi kusema kuwa, pindi mwanadamu unapoanza kuwaza kuwa ni jambo gani utafanya endapo utafeli katika jambo Fulani, ndio wakati huo ambao unakuwa umefeli. Ingawa msemo huu una maana nyingi kulingana na mtu anavyouchukulia, lakini mimi nitapenda niulinganishe na ile misemo tuliyoizoea ya kujipa moyo kwa kila jambo kwani imani tunayojipa ndio hutuongoza kushinda.

Kiasili na kimantiki, matatizo ni kitu chenye kuhitaji utatuzi, wakati ambapo changamoto ni jambo lenye kuhitaji kukabiliwa. Hii maana yake ni kwamba, kufikiri kuwa kila kinachokutokea wewe ni tatizo, kunakuweka katika hali ya ugumu zaidi wa kuweza kuyatatua. Lakini ikiwa utachukulia kuwa kila kilicho mbele yako ni changamoto, ni wazi kuwa utajipa nguvu ya kuzikabili, na humo humo katika kukabiliana nayo, ndipo unapoibuka na mbinu mpya za kuyakabili maisha.

Acha kufikiri kuwa una matatizo, kwani matatizo huhitaji kuyaangalia kwanza na kuyaandalia mikakati ya kuyatatua, na katika maisha hii maana yake ni kuwa muda unazidi kwenda mbele. Lakini kuyakabili kama changamoto, kunakupa mbinu, ujasiri, mwanga, na mwongozo wa kuweza kufikia mahali ambako huenda ni pazuri zaidi kuliko kule ulikokuwa unawaza mwanzoni.

> USIANGUKE, BALI UKWAME.
Gari linapoanguka, aghalabu ni mara chache sana ambako unaweza kumkuta dereva au abiria wakihangaika kulirejesha katika hali yake ya kusimama imara. Lakini shuhudia gari lililokwama, iwe kwenye tope, mlima au popote pale. Utashuhudia namna ambavyo watu wanatokwa na jasho kulisukuma, kutupia mawe, majani, kuchimba njia nk, ilimradi liweze kutoka.

Hii maana yake ni kuwa, pale unapojikuta kuwa umeporomoka kimaisha, au umeshindwa kufikia lengo ambalo ulijiwekea katika maisha yako, ni vyema ukaichukulia hali hiyo kama kukwama tu, na si kuanguka. Hili litakupa nguvu ya kubadili mbinu za kukabiliana na jambo hilo, badala ya kuachana nalo kusubiri msaada wa kuanza tena jambo jingine.

Uzoefu unaonyesha kuwa, wengi wa walioendelea na mipango yao licha ya kukwama mara kwa mara na kukabiliwa na vikwazo mbalimbali, waliweza kufanya vyema zaidi kuliko wale ambao waliacha na kuanza mambo mengine.

>HUJACHELEWA.
Limekuwa ni jambo la kawaida sana kumsikia mtu akizungumzia kuhusu “kwenda kwa muda”. Jambo hili sio tu kuwa limekuwa likiwapelekea watu wengi kufanya mambo kwa papara na kujikuta wakijiharibia zaidi, bali pia limesababisha watu wengi kushindwa kufikia kile walichokuwa wakikiota, kukiwaza au kukitaraji.

Hivi ni nani aliyekuambia kuwa ni lazima uwe umemiliki nyumba ufikapo miaka Fulani? Ni nani au maandiko gani yanasema ni lazima mtu akiwa amefikia umri Fulani awe ameshaolewa? Ni nani aliyesema kuwa kwenye maisha kuna kuchelewa? Huu ni aina ya upuuzi ambao hutakiwi kuuendekeza.

Ni bahati mbaya sana kuwa wanadamu tumekuwa mahodari sana wa kuchukulia kitu mafanikio kama kulingana na Fulani. Nasema ni bahati mbaya kwasababu hakuna mwenye kuwaza hivyo ambaye aliwahi kumfikia Yule ambaye alikuwa anajilinganisha naye na kutaka awe sawa naye. Kwasababu wakati wewe unamfutata, yeye anazidi kusonga mbele zaidi.

Acha kufuata nyayo za mtu mwingine, wala kufuata kasi yake, kwani huko ni kujiumiza zaidi. Tengeneza njia yako mwenyewe, waache wengine ndio wafuate nyayo zako wewe. Na kwa kadiri unavyozidi kuvuta pumzi, amini kuwa hujachelewa, kwani hakuna ambaye ameyawahi maisha. Maisha ni vile unavyoishi wewe na mafanikio ni wewe kuwa au kufikia kile ulichokuwa ukikiota au kukihangaikia.

Badilika sasa. Ishi kwa furaha, furahia maisha. Wewe ni wewe, na hakuna mwingine kama wewe katika ulimwengu huu, jivunie hilo na umshukuru Mungu kwa kukuruzuku maisha hadi hapo ulipo.
Share on Google Plus

About Rama Msangi

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

2 maoni:

luihamu said...

samahani fungua kurasa ya kuchangia mawazo kuhusu jumuiya ya wanablogu tanzania.

http://blogutanzania.blogspot.com/

www.ringojr.wordpress.com

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

nimepitia hapa kucheki na nimeifagilia makala hii iliyokaa kiutambuzi.

kazi nzuri