side ads

Ufunuo wa Nabii Msangi-Mdogo...sehemu ya kwanza

Wapendwa wasomaji wa Jukwaa huru la Uchambuzi, napenda kuwatangazia rasmi kuwa hatimaye mchambuzi wenu NIMEFUNULIWA.Ama! mwashangaa nini sasa? Najua hili litawapa shida wale wenye kunena katika lugha za mataifa, kama kina Martha Mtangoo, Hudson Kazonta, Rashid Mkwinda.....kina Halima Lutavi, Happiness Katabazi na wengineo kadhaa.

Lakini naamini wale tunaonena kwa pamoja katika lugha kiimani, kina Reginald Simon, Ndesanjo Macha, Maggid Mjengwa, Ansbert Ngurumo, Hawra Shamte.... kina Luihamu Lui, Freddy Macha.... kina Amandus Mtani na wengineo wengi, tutakuwa tunaelewana.

Naam.. ndugu zangu tunaonena katika lugha ya pamoja, kama nilivyowaeleza hapo juu, mwenzenu nimefunuliwa. Na zifuatazo ni aya katika ufunuo wa Nabii Msangi-Mdogo.

Nimefunuliwa kwamba, katika miaka hiyo ya eighteen au nineteen forty kweusi, Mungu aliumba bustani nzuuuri sana aliyopenda iitwe Tanganyika na hatimaye Tanzania baadae, kwa uwezo wake. Kwamba katika bustani hiyo akaweka kila kitu alichoona kinastahili kuwepo, kuanzia vito vya thamani, pwani zenye kuvutia, maji ya kila aina na hata ardhi yenye rutuba.

Kwamba katika bustani hiyo, aliweka wanyama wa kila aina na wenye uzuri wa kila aina pia. Akaweka milima na mabonde, ardhi yenye rutuba, na hali za hewa za kila aina. Akaweka Azimio la Arusha, sera za ujamaa na kujitegemea, umoja, mshikamano na amani. Kifupi akaweka kila alichoona kuwa kinampendeza yeye kama Muumbaji.

Baada ya kuridhishwa na uumbaji wake huo, Mungu akaona ainakshi bustani hiyo kwa kuweka viumbe hai, watakaofaidi kila kilichomo katika bustani hiyo. Na kwakuwa bustani hii ilikuwa kubwa zaidi ya ile ya Eden, na kwakuwa bustani hii ilikuwa na rasilimali nyingi zaidi kuliko ile ya Eden, basi Mungu akaona haina haja ya kuweka mtu mmoja na kisha amnyofoe mbavu ili kumpatia mwenza wake.

Kwa mantiki hii basi, akaona kuna haja ya kuwa na watu wengi zaidi kuliko ilivyokuwa kule Eden. Ndipo hapo akawaweka akina Daniel Yona, Basil Mramba...kina Ben William Mkapa, JK, Lowasa, Nizar Karamagi...kina Reginald Simon na wengineo wengi kwa mujibu wa utashi wake.

Basi siku ikapita hivyo na zingine zilizofuatia pia. Dunia ikawa inazidi kulisongesha kiaina ilimradi jua linachomoza, jua linazama na siku zinasonga. Hatimaye siku ya siku Mungu, baada ya kuona kuwa hawa jamaa wame-relax sana, wanafurahia kila kilichomo kwa mujibu wa uumbaji wake, akaona awape mtihani wa kuwajaribu juu ya imani yao kwake. Na njia muafaka ya kuwajaribu akaona ni kuwaletea nyoka mmoja ambaye alimpa jina la madaraka.

Ikumbukwe kuwa kule katika Eden, kulikuwa na watu wawili tu, ambao ni Adam na Hawa. Kwahiyo nyoka yule mmoja tu wa kawaida kama hawa tunaowaona misituni mwetu hivi sasa, alitosha kuwapima imani Adam na Hawa. Lakini katika bustani kuuuubwa ya Tanganyika au Tanzania hivi sasa, kwakuwa kulikuwa na watu wengi pia. Mungu aliona ni vyema akaleta nyoka mwenye uwiano na bustani hii.

Basi akamleta nyoka huyo Madaraka, akiwa na vichwa kadhaa kwakuwa wajaribiwao pia alikuwa kawaweka katika wingi kiidadi. Nyoka huyu akawa na vichwa hivyo vingi kila kimoja kikiwa na jina lake, na majina ya vichwa hivyo yalikuwa Tamaa, Uchu, Uroho, Kukosa utu, Ubinafsi, Kiburi, Dharau, Unafiki, na vingine vingi.

Kwa bahati mbaya kama ilivyokuwa katika bustani ya eden, kuwa nyoka yule aliyeitwa shetani au ibilisi alifanikiwa kuwaingiza majaribuni binadamu wale, nyoka huyu Madaraka naye akafanikiwa kuwaingiza Watanzania katika dhambi kuu. Dhambi ambayo ilimfanya Mungu kushisha laana katika bustani Tanzania.

Na ni hapo Mungu akasema “Mtaishi kwa taabu, umasikini, mateso na mkizidi kupoteza uelekeo kila kukicha kwasababu ya tamaa, uchu, ubinafsi na dharau mlizojijengea. Mtaishi kwa kudharauliwa, kukashifiwa, kutukanwa, kupigwa mawe, kulaaniwa na kila aina ya balaa litawakumba”

Haiyumkiniki. Ndio maana hali si shwari ndani ya Bustani ya Tanzania. na kitabu cha kwanza cha ufunuo wa nabii Msangi-Mdogo, kinafungwa hapo. Je, nini kinafuatia katika ufunuo huu? Kaa mkao wa kusubiri, maana muda si mrefu aya zinaendelea.
Share on Google Plus

About Rama Msangi

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

2 maoni:

HALS said...

Mmmmhhhhhhhhh.........haya Nabii Msangi-Mdogo,sina comment kwa sasa ngoja nisubiri muendelezo wa ufunuo huu mpya utuhusuo wana-danganyika halisi.

Bwaya said...

Ndugu mwenyekiti karibu sana kwa mara nyingine. Wengi nadhani hawakuwa wanajua kuwa umehamia hapa.

Kwa kutambua kuwa hivi sasa wapo wanablogu wapya wengi, nimeweka kibao pale kwangu ili wajue mwenyekiti wao yuko wapi.

Kila lililojema.