side ads

Ufunuo wa nabii Msangi-Mdogo 2... NIJIVUNIE KUWA MTANZANIA

Nianze kwa kuwashukuru watendaji wote wa hili shirika letu la ugawaji wa giza nchini (kifupi chake mtanisaidia maana hata mie sikijui), kwa maana kama si wao kutugawia wakazi wa Mbeya, giza la kutosha, huenda ufunuo huu nisingeweza kuupata.

Basi ndugu zangu, licha ya Mungu kushusha laana kutokana na matendo ya waja wake yaliyoainishwa katika sehemu ya kwanza ya ufunuo wangu, nimeendelea kufunuliwa kuwa natakiwa kujivunia kuwa Mtanzania, licha ya kila linalojiri katika nchi yangu.

Nimefunuliwa kuwa, natakiwa kujivunia kuwa Mtanzania kwakuwa nchi yangu hii ninayoipenda sana, ni nchi ambayo sio tu kuwa ni ya kipekee miongoni mwa zote zilizoko duniani, bali pia, upekee wake ni wa kipekee pia.

Nimefunuliwa kuwa nchi yangu ni ya kujivunia sana kwakuwa ndio nchi pekee ambayo upendo hauwezi kuonyeshwa kwa kushangiliwa, kukumbatiwa wala kupigwa mabusu, bali kwa kupopoana mawe na kuvamiwa njiani.

Nimefunuliwa kuwa nchi yangu hii ndio pekee ambayo wenye dhambi huwa wa kwanza kuwarushia wenye dhambi wenzao, tofauti na enzi za akina nabii ambako utaratibu ulikuwa ni wa asiye na dhambi kuwa wa kwanza kurusha jiwe katika kuwahukumu wale wenye dhambi.

Nimefunuliwa kuwa nchi yangu ndio pekee ambayo kila kitu kipo, kuanzia rasilimali vitu hadi rasilimali watu, lakini watu wake ni masikini sana na wasioweza kunufaika na vitu vilivyowazunguka.

Nimefunuliwa kuwa Tanzania ndio nchi ya pekee ambayo mtu unaweza kuja ukiwa umebeba nguo na mazagazaga yako mengine katika mfuko wa rambo, lakini siku ya kuondoka ukaondoka ukiwa umebeba utajiri katika masanduku ya dhahabu.

Nimefunuliwa kuwa Tanzania ndio nchi pekee ambayo uchumi wake umekuwa unakua kwa kasi kila mwaka, kwa kadiri ambavyo hali za wananchi au wakazi wame ambao ndio wenye kustahili kunufaika na ukuaji huo, zinavyozidi kuwa mbaya.

Kwamba natakiwa kuendelea kujivunia kuwa Mtanzania kutokana na upekee wake ambako sekta inayoajiri sana na inayochukuliwa kuwa uti wa mgongo, ndio ambayo haichangii jambo lolote la maana katika uchumi wa nchi hii.

Nimefunuliwa kuwa natakiwa kuendelea kuipenda nchi yangu kwakuwa hata kama nikiwa mwizi, bado naweza nisichukuliwe hatua, kwa maana nchi yangu hii niipendayo, ndio nchi oekee ambayo wezi huruhusiwa kushikilia sekta muhimu za uchumi, ili wakibainika wasiweze kushtakiwa kwakuwa uchumi utayumba.

Kwamba nchi yangu hii ni ya upekee kwani ndio nchi ambayo fedha nyingi hutumika katika makongamano, tume na uandaaji wa ripoti na uandaaji wa mbinu za kuzihifadhi kwenye makabati yenye vumbi, kwakuwa viongozi hawana muda wa kuzifanyia kazi.

Nimefunuliwa kuwa, nchi yangu hii ndio pekee ambayo kwa kadiri imani zinavyozidi kuwajaa watu mioyoni mwao, ndiovyo ambavyo na maovu yanaendelea kujitokeza. Yaani kiwango cha ukuaji wa imani za kidini za watu ni sawa na ukuaji wa maovu na kinyume chake.

Kwamba nchi hii ndio pekee ambayo sera za mdomoni ndizo zenye kuiongoza nchi na wala sio zile zilizoko katika makaratasi ambayo huitwa vipeperushi.

Nimeelekezwa kuendelea kujivunia kuwa Mtanzania kwakuwa ni katika nchi hii tu ambako matatizo makubwa ya watu huweza kujibiwa kwa majibu ya rejareja, rahisi na yenye kuambatana na tabasamu, ilhali wenye shida hizo wakilia.

Kwamba ni katika Tanzania pekee ambako sehemu kubwa ya bajeti za idara, wizara na ofisi mbalimbali huelekezwa katika mikutano, ziara, warsha na posho badala ya masuala ya kimsingi yanayotakiwa kuratibiwa na sehemu hizo.

Kwamba ni katika nchi hii tu ambako ukweli huweza kugeuzwa kuwa uongo, mtu akiambiwa yuko uchi anaweza kujitetea kwa kusema wanaomwambia hivyo ni majungu na akaendelea kupuyanga mitaani sehemu ya makalio yake yakiwa nje, kwakuwa hajali watu wanasema nini au yeye ni nani.

Nimefunuliwa kuwa, kwa kadiri giza litakavyokuwa linaendelea kuwepo mkoani Mbeya, ndivyo ambavyo nitaendelea kufunuliwa, kwahiyo muendelee kukaa mkao wa kusoma aya zaidi za ufunuo wangu.
Share on Google Plus

About Rama Msangi

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni: