side ads

Siku ya haki za binadamu duniani... TANZANIA tuna nini cha kuadhimisha.

Leo ni maadhimsho ya siku ya haki za Binadamu Duniani. Ikiwa ni kumbukumbu ya siku ambayo Umoja wa Mataifa ulipitisha tamko la Haki za Binadamu, mwishoni mwa miaka ya 1940.

Tamko la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu, ni moja kati ya matamko ya Umoja huo yenye historia ndefu sana, na ambayo yameweza kuleta changamoto kwa nchi mbalimbali wanachama wa Umoja huo toka lilipotolewa miaka hiyo. Soma haki za msingi za binadamu kwa mujibu wa tamko hilo kwa kubonyeza hapa.

Ingawa Tanzania, ikiwa mmoja wa wanachama wa Umoja wa Mataifa, katika siku ya leo ilijiunga na mataifa mengine katika kuadhimisha hii, mimi kama mmoja wa Watanzania, nimekuwa najiuliza, hivi tuna haki au jambo gani hasa la kuweza kutufanya tujumuike na Mataifa mengine katika kuadhimisha siku hii.

Ndio. Kuna jambo gani hasa ambalo tunaweza kusema eti linatupa sifa ya kujumuika na wenzetu katika kuadhimisha siku hii, ilhali maisha yetu yameendelea kuwa kama ya wakimbizi ndani ya nchi yetu?

Wananchi wamekosa makazi bora, nyumba za wananchi zimekuwa zinavunjwa bila sababu zenye kuwaingia watu akilini, zaidi ya kuwa wakuu wa nchi wamejisikia iwe hivyo, sasa kuna haki gani ambayo tunatakiwa kuisherehekea hapo?

Vijana wetu ambao ndio nguvu kazi ya nchi hii kwa makusudi kabisa wamekuwa wakinyimwa haki yao ya msingi, ambayo ni elimu kwa kisingizio kuwa serikali haina fedha, wakati wakubwa wakizidi kubadili magari ya kifahari, kuendelea kuongezana posho na wengine wakiiba fedha za umma. Kuna haki ipi ya kusherehekea hapo?

Huduma hii muhimu imebidhaifishwa na wakubwa wetu wenye tamaa ya kujipatia fedha za haraka haraka. Wameamua kujianzishia shule maalum na kuweka viwango vikubwa vya ada, kwa ajili ya watoto wao, ilhali wale wa maskini wakiendelea kusotesha makalio katika matofali, na wanapomaliza wananyimwa nafasi za kuendelea. Kipi cha kutufanya Watanzania tuadhimishe siku hii?

Huduma za msingi kwa wananchi kama maji na umeme, zimeendelea kuwa kitendawili kwa asilimia kubwa ya Watanzania. Nyaya za umeme zimeendelea kuwa juu zaidi ya makazi ya walalahoi kuliko ilivyokuwa awali, huku nyumba za masikini zikiwa wahanga wa kubomolewa nyumba ili mabomba ya kupelekea maji kwa wakubwa yaweze kupitishwa. Kipi hasa watu hawa wanatakiwa kukichukulia kama kigezo cha kuadhimisha siku hii?

Huduma za afya, zimebidhaifishwa, wakuu wakiendelea kukimbilia nje kwa matibabu pindi wanapoumwa, kupeleka watoto wao hukohuko wakatibiwe, huku mama zetu wakiendelea kufa sababu ya kukosa huduma nzuri za uzazi katika mahospitali yetu. Kipi hasa wajivunie katika siku hii?

Mauaji ya ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi yanazidi kushamiri, huku juhudi kubwa ambayo inafanywa na viongozi wetu ikiwa ni ile ya kupayuka majukwaani eti kukemea tabia hiyo, na kukazana kuwaalika katika makongamano mbalimbali. Kipi hasa wajivunie ndugu zetu hawa katika siku hii?

Haki za wafanyakazi zimeendelea kuchukuliwa kama ruzuku, ambayo serikali inaweza kutoa pale inapojisikia, hivyo wafanyakazi wa kada mbalimbali za chini wakiendelea kuwa hoi kila uchao. Wajivunie lipi wafanyakazi hawa katika siku hii?

Matumizi ya nguvu za dola katika kudhibiti ushamiri wa demokrasia, yameendelea kukua kila kukicha tofauti na matamshi yanayohanikizwa majukwaaji na viongozi wetu, wakati demokrasia hasa ya kutoa maoni ni moja ya haki nyingi za msingi za mwanadamu. Mtanzania ajivunie nini katika siku hii wakati hana hilo?

Mie nina mengi sana kwakweli ambayo yananifanya nione kuwa Watanzania hatuna lolote la kujibaraguzia eti tunajumuika na watu wa mataifa mengine katika kuadhimisha siku hii....... wewe una yapi ambayo unadhani yanakufanya uone una haki ya kuadhimisha siku hii?
Share on Google Plus

About Rama Msangi

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

2 maoni:

Yasinta Ngonyani said...

kwa kweli ukiangalia kwa kina kirefu inasikitisha sana kwani wenye haki hawana kiti na wasio na haki wanapata vyote kwa hali hiyo itabidi viongozi wabovu waondolewe madarakana na tunapochagua viongozi wengine tuchagua kwa makini si ila mradi tumechagua basi tutakuwa hatuna haki hadi dunia hii itakapokwisha kama itakwisha.
Ni hayo tu kazi kwelikweli!!

Mzee wa Changamoto said...

Kaka upo? Twakuombea mema popote ulipo mkuu