side ads

TUMEKUSIKIA MHESHIMIWA PINDA, LAKINI SIJUI KAMA TUMEKUELEWA

Miongoni mwa mambo ambayo mh. Mizengo Pinda, aliyazungumzia kwa kina katika hotuba yake ya kuahirisha kikao cha 13 cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lilikuwa hili la huu utamaduni unaochanua kwa kasi sana nchini mwetu, utamaduni wa migomo na maandamano.

Waziri mkuu huyu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alitumia muda wa kutosha kuelezea, tena kwa mistari iliyonyooka, athari zitokanazo na utamaduni huu, ikiwa ni pamoja na kukosekana kwa huduma muhimu hasa inapotokea kuwa wahusika wanatoka katika asasi zinazoshughulisha na utoaji huduma.

Hakusahau kusema kuwa, kila inapotokea mgomo au maandamano, kwa kawaida wahanga ama waathirika wakubwa wa migomo na maandamano hayo ni wananchi wa kawaida ambao yeye alidai wengine wao wala si wadau wa kile kinachodaiwa na wagomaji au waandamanaji.

Na wala hakusahau kueleza namna amani na mshikamano vinavyoweza kuvunjika kutokana na kushamiri kwa utamaduni huu, na kama ilivyotarajiwa, akahitimisha kwa kusema kuwa serikali haitovumilia kuona utamaduni huu unazidi kustawi, hivyo serikali itajitahidi kuudhibiti.

Ukiachilia mbali kauli aliyoitoa wakati fulani kuhusiana na kigugumizi cha serikali kuwafikisha mahakamani wezi wa fedha za EPA, kuwa serikali inahofia kubwagwa na hao jamaa kwa kuwa wana fedha, ambayo ilikuwa ni sawa na serikali kukiri kuwa humu nchini fedha hununua haki, kauli ambayo hadi leo naamini aliitoa kwa kukengeuka, kwa ujumla, mhe. Pinda, hukupenda kujipambanua katika hotuba na utendaji wake.

Ndio maana leo hii napenda kumpongeza kwa hotuba ile, lakini sidhani kama tunatakiwa kukubaliana nayo hasa katika kipengele kile cha serikali kujipanga kudhibiti hali hii kwa kutumia vyombo vya usalama. Hebu tujadili hapa.

Ikiwa tayari imeshajijengea umaarufu kutokana na staili yake ya kuundia kila tukio tume, kiasi cha kupachikwa jila la Awamu ya Tume, awamu hii ya utawala chini ya Mheshimiwa Jakaya Kikwete, katika siku za karibuni imekuwa inakabiliwa na changamoto ya wananchi walio wengi kujua haki zao njia mbalimbali za kuzidai zinapokawizwa.

Na miongoni mwa njia muafaka ambazo zinazotumiwa ni hizi za maandamano na migomo. Tumesikia kuhusu mgomo wa walimu, ambayo licha ya serikali kuuzuia mahakamani, lakini ungali ukifukuta, migomo katika Vyuo Vikuu, mashirika kama vile TRL, NMB na mengineyo, migomo katika taasisi za serikali kama Muhimbili na mingine kadhaa.

Tumeshaona maandamano ya wanafunzi kuanzia wa shule za msingi hadi vyuo, waandishi wa habari, ndugu zetu Albino, na mengine kadha wa kadhaa. Yote haya yametokea kwa kasi sana katika mwaka huu ambapo awamu hii imefikia nusu ya utawala wake wa miaka mitano.
Kama alivyosema waziri mkuu, matukio haya kwa ujumla wake, yamekuwa ni yenye athari kubwa sana katika jamii nzima kwa ujumla. Ziwe ni athari hasi ama chanya, lakini zimejitokeza kwa ujumla wake na zimeonekana, ingawa sina hakika kama zimeweza kuwa ishara ya awamu ya nne kujitambua kuwa imeshindwa kutimiza wajibu wake kwa wananchi kikamilifu.

Ndio, nasema kuwa imeshindwa kutimiza wajibu wake kikamilifu, hasa kwa kuzingatia ahadi ilizokuwa imezitoa wakati ikiomba kura, kwakuwa penye utatuzi wa matatizo ya wananchi na hasa nchi yenyewe inapokuwa ni Tanzania, wananchi wake si watu ambao wanapenda kufanya mambo ambayo waziri mkuu anayaita yenye kuhatarisha amani na mshikamano baina yetu.

Kimsingi, kile ambacho nilitarajia katika hotuba ile, kilikuwa ni kumsikia mheshimiwa Pinda, akielezea chanzo cha migogoro hiyo, viongozi wanaoisababisha na hata hatua ambazo wamezichukua dhidi yao. Hivi mgomo wa wafanyakazi wa NMB. Ulisababishwa na wafanyakazi hao kudai haki yao au viongozi ambao wamekujihalalishia mfumo wa wao kujali maslahi yao zaidi kuliko ya wengine?

Si tunaambiwa kuwa viongozi wa vyama vya wafanyakazi walifanya kikao na viongozi toka wizara ya kazi na maendeleo ya vijana, wakafikia makubaliano, lakini watu kutoka hazina wakagoma kutia sahihi makubaliano hayo ambayo yangewezesha wafanyakazi wale kulipwa na kutuliza mizuka yao?

Waziri Mkuu, hapa angetueleza kuwa ni hatua gani ambayo waliichukua dhidi ya wale wanaodaiwa kuwa waligoma kutia sahihi makubaliano ambayo yalikuwa yamefikiwa baina ya serikali na viongozi wa vyama vya wafanyakazi, kwakuwa yalikuwa ni maamuzi yaliyokubaliwa na serikali.

Huu ni moja tu ya mifano ambayo nilitarajia kuwa mheshimiwa Pinda angeuchukulia kama ishara ya kukosekana kwa uadilifu miongoni mwa watendaji waliopewa dhamana katika sehemu mbalimbali, na akatueleza kuwa wanawafanya nini viongozi wa namna hii.

Ikiwa hali ilikuwa hivyo kweli, Waziri Mkuu alitarajia nini hasa toka kwa wafanyakazi wale? Kuwa wakae kimya katika sehemu zao za kazi wakati punguani mmoja anaamua kukataa kukubali kuwatendea haki yao, na serikali inamtizama tu? Kisha aje atuambie kuwa eti watu wa namna hiyo watakuwa wakidhibitiwa na serikali kwa kutumia nguvu zake za dola?

Hivi madhara ambayo jamii inayapata kutokana na utendaji mbovu wa viongozi tuliowachagua na kuwaamini, yanadhibitiwa kwa njia gani hasa? Au vyombo vya dola vipo tu kwa ajili ya kuwadhibiti wananchi, hata kama kile wanachodai ni haki yao?

Nilichokitarajia kutoka kwa Mhe. Pinda, katika hotuba yake, ilikuwa ni kusikia watu wangapi wamechukuliwa hatua kutokana na uzembe wao kusababisha kuchelewa kuhakikiwa kwa madai ya walimu hadi wakafikia hatua ya kutangaza mgomo ambao serikali iliamua kukimbilia mahakamani kuutuliza.

Lakini pia, kulingana na uzoefu ambao umejionyesha ni kuwa, migomo au maandamano mengi yamekuwa yenye manufaa kwa wale waliokuwa wakidai haki yao kwa njia hiyo. Hii ikimaanisha kabisa kuwa, serikali yetu imeridhia kuwa haiwezi kufanya kazi bila kushinikizwa.

Na kama wananchi wamekuwa wakishuhudia namna ambavyo mashinikizo toka nje yamekuwa yakifanyiwa kazi haraka na wahusika kutimiziwa kile wanachokitaka, kwanini nao wasitumie mfumo huo huo wa kuishinikiza serikali yao katika kudai kilicho halali yao?

Wanafunzi mara kadhaa wamegoma, wameandamana, na kisha serikali ikasikiliza kile wanachokitaka, japo hawajatimiziwa yote, lakini walau wanaweza kujivunia kuwa yapo ambayo yalishawahi kufanyiwa kazi.

Matukio yote haya, ni ishara za udhaifu mkubwa sana serikalini. Ni ishara ya uzembe na uozo ambao umejaa katika vyombo mbalimbali vyenye kuhusika na kuhakikisha kuwa mambo yanakwenda katika mistari iliyonyooka. Ni ishara ya kuwa kada mbalimbali za uongozi, zimejaa mabwanyenye ambao hawafanyi kazi hadi kusukumwa. Kifupi ni ishara ya kuwa tuna genge la viongozi ambao kufanya kwao kazi ni hadi kwa mjeledi kama punda.

Hebu fikiria kuwa suala la walimu lilichukua muda gani kwa kile kilichokuwa kinaitwa kuhakikiwa kwa nyaraka zao? Zilikuwa zinahakikiwa na akina nani? Maana kama kila mkoa ungekuwa unawajibika ipasavyo na kwa uadilifu, uhakiki huo kilitakiwa kiwe kitu cha kufanyika katika mikoa yao na inapofika makao makuu ni kwa ajili ya kulipwa tu. Na kwa mpango huo, wala haikuwa kazi ya kumchukua mtu mwezi mzima kuimaliza.

Tatizo ninaloliona hapa na ambalo ni tatizo kubwa sana kwa watendaji wetu katika nafasi mbalimbali, ni kukosekana kwa maadili. Viongozi wa ngazi za chini hawaaminiwi kwa kazi zao kwakuwa hutumia mianya ya namna hiyo nao kuingiza taarifa zilizo za uongo ili kujinufaisha. Na wakipeleka juu nako si kuwa eti zinahakikiwa, bali ukweli ni kuwa zinazidi kuongezwa taarifa za uongo ili wakubwa nao wapate mahali pa kulia.

Kwa maana uhakiki huo sanasana naweza kusema unalenga zaidi katika kubaini mianya iliyokaa wazi kwa ajili ya watu nao kupenyeza ujinga wao wa madai hewa, ili wachume fedha za wananchi, badala ya kuondoa hata ile iliyopo. Ndio maana siku zote serikali yetu imekuwa ikilipia madeni hewa, licha ya kazi za uhakiki kuchukua miaka wakati mwingine.

Na kwangu mimi, ni bahati mbaya sana kuwa mhe. Pinda, alishindwa kutueleza hili Watanzania. Alishindwa kukiri kuwa kuna mapungufu makubwa ya kiutendaji katika jopo linalowajibika kwake, hali ambayo baadae itamsababisha naye kuonekana mtu asiye muwajibikaji, tofauti na wananchi wengi walivyokuwa wakimuelewa.

Serikali kukimbilia mahakamani, kuzuia maandamano ya walimu, kutishia kutumia vyombo vya dola katika kudhibiti migomo na maandamano, ni ishara ya wazi ya kushindwa kwake kuwaletea Watanzania, maisha bora ambayo waliyaahidi, na badala yake kuishia kuwa serikali ya blah blah nyingi na siasa.

Wafungwa wamekuwa wakihenyeshwa katika kesi zao hadi kufikia kufanya migomo, ukiuliza chanzo, uchunguzi kutokukamilika. Lakini uchunguzi huo unashindwa kukamilika huku maaskari wakiwa wanazagaa mitaani tu na kukimbizana na wauza ndizi ambao wanajitafutia rizki kihalali.

Unashindwa kukamilika wakati mwingine kwa madai ya kukosekana kwa usafiri, huku mashangingi ya waheshimiwa yakiwa yanazurura mitaani, kupeleka watoto wa vigogo shule, wake zao magengeni na hata sehemu za starehe, tena kwa kutumia mafuta ya serikali yatokanayo na fedha za umma.

Kisha mhe. Waziri Mkuu, anataka kutuambia kuwa watu wa namna hii wanavunja amani!! Ni vyema mhe. Pinda, akaitizama upya kauli yake hii kwakuwa siamini kama imelenga katika kuhakikisha amani na utulivu vinakuwepo, bali kuharibu zaidi mambo.

Maana sitarajii kama kuna mtu atajali kupambana na hivyo vyombo vya dola au usalama, wakati akiwa anadai kile ambacho anaona ni haki yake, na ambacho kimsingi kweli ni haki yake.

Sitaki na wala sipendi tufike huko, lakini ukweli ni kuwa, ikiwa hali itaendelea hivi kwa maana ya utendaji mbovu wa viongozi kuendelea kukua na kuchanua, maandamano na migomo ni wazi havitasimama leo wala kesho. Na ni wazi kabisa kuwa watu watafanya hivyo nao wakiwa wamejiandaa kukabiliana na hivyo vyombo vya dola, na hapo ndipo hali itakuwa mbaya zaidi.

Kudhihirisha kuwa wananchi wanapofanya hivyo wanakuwa na haki, ndio maana mara zote ambapo wamethubutu, kilio chao kilisikilizwa, na ndio maana ni asilimia ndogo sana ya Watanzania, ambao unaweza kuwasikia wakipinga maandamano na migomo, kwakuwa wengi wanajua wazi kuwa madai yanayotolewa na hao watu, hata kama hawawatibu wakati huo, au hawawafundishi kwa wakati huo.

Hivyo basi, kuna umuhimu wa serikali kuangalia upya juu ya kauli hii na matokeo yake, kisha ndio itamke wazi kuwa ianze kutumika au laa.

.....nawasilisha.......
Share on Google Plus

About Rama Msangi

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni: