side ads

Tatizo ni OIC na Mahakama ya Kadhi au sisi wenyewe?

Niliwahi kuandika huko nyuma (hebu acheni upuuzi huo, simaanishi nyuma mnayodhania nyie, maana hata rais aliposema kula uliwe, watu walishangiliiiiia kama hawana akili vile) kuhusiana na kuyumba, kama si kupoteza uelekeo kwa viongozi wetu wa kidini. Ikiwa wewe ni mmoja kati ya waliokosa kusoma kile nilichoandika wakati huo, basi bofya hapa kusoma.

Si nia yangu kurejea makala ile, wala si nia yangu kuandika eti kwakuwa Mungu huwa hasomi blogi, kama alivyosema kaka yangu RS Miruko, bali nimevutika kuandika (kwa mara nyingine tena), kuhusu masuala yenye kuhusisha imani, kutokana na hii filamu ya OIC na Mahakama ya Kadhi, ambayo inaendelea hivi sasa nchini.

Hizi ni filamu yenye kuhusu masuala ya kiimani, masuala ya kidini, na ambayo katika kipindi fulani mheshimiwa Benard Membe, alionekana kama ndiye staring wake na akateka hadhira ya Watanzania kwa kiasi kikubwa kabla ya kupikuliwa na staring mwenyewe, mheshimiwa JK, ambaye uigizaji wake ndio umeifanya isuesue kitaarifa.

Naam! Ni OIC na Mahakama ya Kadhi, filamu ambazo licha ya kujizolea umaarufu siku za karibuni, lakini zilichezwa na kuingia mitaani katika zama zile ambazo upande wa pili wa Tanzania, kwa maana ya Visiwani Zanzibar, ulikuwa chini ya Komandoo aliyejulikana kwa jina la Dk. Salmin Amour, na ambaye ndio alikuwa staring wake.

Ukijaribu kufuatilia kwa kina majadiliano na makumbano ambayo yamekuwa yakiendelea kila kona kuhusu suala la IOC na Mahakama ya Kadhi, ni wazi kuwa kuna mambo matatu ambayo utaweza kuyabaini kwa kinaga ubaga. Mambo hayo ni pamoja na viongozi wa dini kusahau wajibu wao wa kuhubiri dini, na badala yake kuwa wahubiri wa masuala ya madhehebu na utengano miongoni mwa jamii.

Kingine ni kuzidi kukua kwa tabia chafu na ambayo nimekuwa nikishangaa ni kwa nini viongozi wa dini wanazidi kuimwagilia ili ishamiri. Nazungumzia tabia ya viongozi wa kisiasa kutumia dini kusaka kile ambacho mimi nilipokuwa pale Magamba Sekondari, tulikuwa tukiita ujiko. na jambo jingine lililo wazi katika mijadala kuhusu OIC na Mahakama ya Kadhi, ni uvivu wa kusoma na kufikiri uliomo ndani ya vichwa vya viongozi wengi wa kidini.

Katika kipindi ambacho suala hili lilitawala sana kurasa za magazeti mbalimbali nchini na vipindi mbalimbali vya radio na luninga, aliyekuwa kinara wa kulihanikiza alikuwa ni Waziri wa Mambo ya Nje, Bw. Benard Membe, ambaye katika baadhi ya nyakati kwa waliowahi kumsikia, alikuwa akiongea kwa kiburi na jeuri fulani hivi.

Cha kushangaza zaidi ni pale siku chache baadae, aliposimama mkuu wa nchi na kuutangazia umma kuwa watu wamekuwa wakilijadili suala hilo kwa njia za jazba zaidi hali ambayo imepelekea kuanza kuashiria kuwa litaleta mtafaruku na kusababisha kuvuruguka kwa amani nchini. (hivi bado ipo amani na mshikamano jamani?)

Malumbano au mgongano huo wa matamko ya viongozi hawa wawili unamaanisha nini hasa? Kuwa serikali yetu imekuwa ikifanya kazi kila mtu na lwake au viongozi wetu wamekaa mkao wa nitoke vipi, hivyo kila linalokuja mbele yao wanaona kuwa ndilo sahihi kutokea?

Kulikuwa na mantiki gani kwa Waziri wa mambo ya Nje, kulishupalia suala hili, kulifanya ajenda yake kuu kila alipoenda hata kama mahali hapo hapakuwa mahali muafaka kulizungumzia? Patamu zaidi ni vile alivyokuwa akitumia vyombo vya habari kufanya kile ambacho naweza kukiita kujibizana na wale wanaoonekana kupinga suala hilo? Kulikuwa na haja gani kwa yeye kufanya hivyo wakati serikali ilishaandaa utaratibu maalum kwa ajili ya kuratibu mchakato wa kujiunga ama kutojiunga na OIC? Tafakari.

Tukiachana na hilo la wanasiasa kutumia dini kama mlango wao wa kutokea, hebu turejeshe fikra zetu kwa kuangalia mjadala huu unavyoendeshwa katika kada ya viongozi wa kidini. Niliwahi kuandika mwaka 2007, kwamba, ninapata tatizo sana kila ninapojaribu kutafakari matendo ya viongozi wa dini mbalimbali nchini na hata sehemu zingine duniani.

Nilieleza kwa kina kuwa, maandiko yote matakatifu hayajawahi kunielekeza kuwa wajibu wa viongozi wa dini ni kuhubiri masuala ya madhehebu, bali kuhubiri uwepo wa Mungu, ukuu na utakatifu wake. Maandiko yoye yanahimiza maisha bora kwa kila mwanadamu (sio maandiko yale ya CCM lakini), kwa njia zilizo sahihi. Yanahimiza juu ya mshikamano wa ulimwengu katika kutenda mema, kumjali na kumuabudu Mungu sanjari na kuwezeshana kila mmoja aishi kwa mujibu wa maandiko hayo.

Kila ninapojaribu kuangalia namna viongozi wetu wanajadili hili suala na hususan wale wa madhehebu ambayo ni mbali ya Uislamu na hata walio waisilamu katika baadhi ya nyakati, nabaini kuwa viongozi wetu wanachokifanya sasa si kuhimiza na kueneza dini. Bali kuhimiza na kueneza mgawanyiko kwa kisingizio cha hivi vitu vinavyoitwa madhehebu. Hivi kama viongozi wetu wote wangeamini katika kutenda mema, kuna haja gani ya kuhofia kuwa fulani akiwa uchi hatoabudu?

Ni kwanini Waisilamu wahofie Wakristo wanaojiunga na Jumuiya fulani kwa lengo la kuwapatia maslahi fulani? Ni kwanini hali iwe hivyo hivyo kwa Wakristo kwa waislamu? Sio kwasababu viongozi hao wamejenga ubinafsi ndani yao na kuwaambukiza waumini wao pia hali hiyo? Hivi kama una mahusiano mazuri na jirani yako, iweje uogope yeye anapoamua kufanya jambo fulani? Kwasababu litawanufaisha nyote wawili.

tabia hii ya viongozi wa dini kujitahidi kila mmoja kuwajengea ubinafsi waumini wake, kwa lengo la wao kujiona bora zaidi kuliko wengine, si tabia ambayo imeainishwa katika maandiko ya dini. Ni tabia ambayo imekuwa ikichangia hiki kinachoonekana kama malumbano ya kidini. Ni tabia ambayo inatokana na viongozi wa kidini kushindwa kutimiza wajibu wao wa kuhimiza uwepo wa Mungu na kwamba yule mwenye kuabudu kwenye kanisa, msikiti, mbuyu, wote lao linastahili kuwa moja midhali wote wanamuabudu Mungu huyo huyo.

Lakini ukiachilia mbali hii tabia ya baadhi ya watu kulumbana suala la OIC kutokana na maslahi ya vichwani mwao tu, suala jingine ambalo nililiainisha hapo awali ni ile hali ya uelewa finyu wa masuala mengi, tatizo ambalo pia wanalo viongozi wengi wa kidini nchini. Sijui kama kuna miongoni mwa wale wanaopinga ambaye ameweza kupitia kwa kina akaijua hasa OIC ni nini, malengo yake na wanachama wake ni kina nani hasa.

Kwanini ionekane kuwa Tanzania ndiko pekee ambako kujiunga na OIC litakuwa tatizo kubwa ambalo litaleta kuvunjika kwa amani na mshikamano? Mbona nchi zingine ambazo zimejiunga hatujasikia kuwa ziliparaganyika kwasababu ya OIC? Hivi OIC ni Jumuiya ambayo ndio itakuwa inaiamulia Tanzania kila kitu kuihusu?

Naomba nishushe pumzi kwanza, nikimbilie kuangalia mechi kwenye luninga yangu maana niliimiss sana kutokana na mkoa wa Mbeya kuwa gizani kwa muda wa zaidi ya wiki. Tujadili kuhusu OIC na sio kulumbana....
Share on Google Plus

About Rama Msangi

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni: