side ads

Kitu gani katika mwanadamu kivutie kupenda?

KATIKA mahusiano ya namna yoyote ile ya kimapenzi, kwa maana ya wapenzi wa kawaida, wanandoa, mahawara nk, kiasili na ilivyozoeleka sehemu zote duniani, mwanaume huwa ndiye mwenye kuyaanzisha mahusiano ya namna hiyo. Kwa maana ya kuwa yeye ndiye humtokea mwanamke na kumuomba kuanza kwa mahusiano hayo.

Hali hii imekuwa ni ya enzi na enzi, imezoeleka na imekuwa kama utamaduni. Ingawa katika miaka ya karibuni utamaduni huu umeanza kugeuka kwa wanawake nao kuwatokea wanaume kwa kigezo cha kuua mfumo dume, lakini ukweli ungali unabaki palepale kuwa kiuumbaji, mwanaume ndiye mwenye kuongoza jahazi hilo la kuanzisha mahusiano ya kimapenzi.

Katikati ya uasili huo, wataalamu wa saikolojia ya binadamu wanatuambia kuwa, wanaume ndio wenye kupenda haraka zaidi kuliko wanawake lakini pia kasi ya wanaume kutoka mapenzini ni ya haraka zaidi pia kuliko wanawake. Kwa maana ya kuwa mwanaume kumwona binti na akampenda hutokea haraka zaidi kuliko kwa mwanamke. Kwa maana ya kuwa mwanaume kuchoshwa na penzi alilomo na kuamua kujitoa ni ya karaka zaidi kuliko upande wa mwanamke.

Ni kwanini basi mtu mwenye kuanzisha akawa pia mstari wa mbele kusitisha kitu hicho hicho alichokianzisha? Hili ndilo jambo ambalo ningependa kuliangalia katika mjadala wa kwanza kabisa kwenye maskani yangu hii ya njia panda za maisha, ingawa pia nina uhakika kuwa sitokuwa mtu wa kwanza kujadili suala la aina hii.

Tafiti mbalimbali zilizofanywa na watu mbalimbali katika kona mbalimbali za dunia yetu hii zinaonyesha kuwa kwa ujumla, wanawake ni viumbe ambao ni wazito sana katika kupenda, lakini pia walio wazito sana katika kutoka kwenye mahusiano pindi wanapokuwa wameyaingia. Hili kitaalamu linaelezeka, na hata katika lugha za wahenga pia linaelezeka. Ndio, si tuliambiwa kuwa achekae mwisho hucheka zaidi!

Kwa mujibu wa tafiti hizo, wakati asilimia kubwa ya wanaume huangalia vitu ambavyo huonekana zaidi katika mwanamke, wanawake hali ni tofauti sana. Unene, wembamba, ufupi, urefu, weupe, weusi wa kung'aa, umbo namba nane, fedha, majumba ya kifahari, kisomo na mambo mengine ya namna hiyo ni baadhi ya vigezo ni vya kawaida kabisa kwa mwanaume kuvizingatia pindi akiwa anachagua mtu wa kuwa naye katika mahusiano.

Kwa bahati mbaya sana, vigezo hivi vimeweza kufanya kazi chanya katika asilimia chache sana ya waliovichagua, huku wengi wao vikishindwa kabisa. Ni rahisi sana kwa mwanamke mnene kuwa mwembamba ikiwa anakumbwa na tatizo lolote la kiafya ambalo litateteresha mfumo wake wa mwili.

Ni rahisi sana kwa mwanamke mwembamba kuwa mnene sana pindi akikosa ratiba maalum ya kuudhibiti mwili wake. Ni rahisi kwa mtu mweupe kuwa mweusi, au mweusi kugeuka kuwa mweupe. Ni rahisi kwa mwanamke mwenye guu la bia kugeuka hana hata hiyo miguu. Ni rahisi sana kwa mtu mchangamfu akageuka kuwa mtu wa simanzi. Ni rahisi kwa mwenye kisomo kufikia mahali anaonekana ana elimu ya kawaida sana.

Kifupi ni rahisi sana kwa kitu chenye kuonekana kwa mwanadamu kubadilika. Kuna mazingira mengi sana ambayo huweza kubadili hali hizo. Zipo sababu za kimaumbile ya kiuumbaji ambapo kwa mfano kuna baadhi ya vitu hupotea kwa mwanadamu kwa kadiri anavyokua na umri mkubwa na mambo mengine ya namna hiyo. Kwa mantiki hiyo basi ni rahisi sana kwa mtu ambaye alikuwa amependa kitu fulani toka kwa mtu huyo, kuchoka na kutafuta njia nyingine pindi kitu hicho kinapotokea.

Wakati hali ikiwa hivyo kwa wanaume, kwa upande wa wanawake, bahati nzuri sana waliyo nayo wengi wao kwa mujibu wa tafiti ni kuwa wao hupenda zaidi mambo yasiyoonekana. Hupenda mambo ambayo yako ndani ya mwanadamu kuliko yaliyo nje.

Utafiti umeonyesha kuwa ule uwezo wa kupenda alionao mwanadamu na hususan mwanaume mara nyingi ndio ambao umekuwa ukiwavutia wanawake wengi. Sasa bahati mbaya sana iliyopo katika muktadha huu ni kuwa, wanaume wengi wamekuwa ni watu wenye kuonyesha kiwango kikubwa sana cha mapenzi katika nyakati zile tu za awali za mahusiano.

Ile hali ya kumnyenyekea wakati wa kumtokea, ahadi unazompatia, matumaini unayompatia, mpangilio wa maneno, huruma, kumjali na mambo mengine kama hayo, ambavyo wanaume hupenda kuyaonyesha wakati wa kumtokea binti yeyote pindi anapokuwa anamhitaji, ndio mambo ambayo yamekuwa yakiwavutia wasichana hadi kukubali maombi ya wanaume.

Moyo wa huruma ni jambo ambalo aghalabu ni vigumu sana kumtoka mwanadamu hasa kama alikulia katika mazingira yaliyomjengea moyo wa namna hiyo. Hali ya kujali, kunyenyekea, kuthamini na nyingine nyingi ambazo kimsingi hutokana na makuzi yetu toka utotoni hadi ukubwani, ni mambo ambayo kwa ujumla wake huwa hayabadiliki kwa urahisi, kama tajiri kuwa masikini au mwembamba kuwa mnene. Na wala hayatafutiki kiurahisi sana kama utajiri nk.

Kwa bahati mbaya sana haya mambo yenye kumvuta mwanamke kwa mwanaume mwenye kumtokea, ndio hayo hayo ambayo wanaume huyasahau haraka sana pindi anapokuwa tayari ameshampata mwanamke huyo. Ni kwanini basi huwa hivi? Mimi na wewe tunaweza kuwa na mtazamo tofauti tofauti sana. Na ndio mitazamo hiyo ambayo napenda tujadiliane kwa kina na kisha tusaidiane haya yafuatayo.

Kuna haja ya wanaume kubadilika nao wakaanza kupenda vitu vilivyoko ndani ya mwanadamu badala ya vitu vinavyoonekana katika mwanadamu? Naomba nifungue rasmi jukwaa la mijadala katika maskani hii kwa kukomea hapa. Wewe unasemaje?
Share on Google Plus

About Rama Msangi

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

1 maoni:

HALS said...

MAMBO NIAJE?
KWA MTAZAMO WANGU NADHANI SI KWAMBA SIKU HIZI WANAWAKE/MABINTI WANAJARIBU KUUA MFUMO DUME PALE WANAPOAMUA KUWA WA KWANZA KUTAKA KUANZISHA MAHUSIANO,MIMI NADHANI NI VILE TU MTU ANAPENDA KUELEZEA HISIA ZAKE KWA YULE AMBAYE MOYO WAKE UMEMDONDOKEA BADALA YA KUSUBIRI ATAMKIWE KWANZA KWASABABU YAWEZEKANA JAMAA HATAKUWA ANAMUONA INGAWA WANAPISHANA KILA UCHAO NJIANI.......KWASASA NADHANI MPANGO UNAOTUMIKA NI ULE WA NGOJA NGOJA HUUMIZA MATUMBO.
NA KWA WANAUME KUTOKA HARAKA KATIKA MAHUSIANO WALIYOYAANZISHA KWA HIYARI YAO,INATOKANA NA KUWA WENGI WAO HAWAPENDI BALI WANATAMANI NA NDIO MAANA AKIONA MGUU TU ANADAI AMEMPENDA MWANAMKE.
NI BAADHI TU YA MAWAZO YANGU........KEEP IT UP