side ads

HATIMAYE SOKO LA MWANJELWA KUANZA KUJENGWA

TAKRIBANI miaka miwili toka kuungua hadi kuteketea kwa moto kwa lililokuwa soko maarufu la Mwanjelwa jijini Mbeya, hatimaye, Halmashauri ya jiji hilo, imetangaza kuwa ujenzi wa soko jipya litakalochukua nafasi ya lile la awali, unatarajiwa kuanza ndani ya kipindi cha miezi sita ijayo.

Tamko hilo lilitolewa jijini Mbeya, mwanzoni mwa wiki, wakati wa utiaji saini mkataba baina ya Halmashauri ya jiji hilo na kampuni ya MD Architecs Consultants, iliyoshinda zabuni ya ujenzi huo, kwa mujibu wa vigezo walivyotakiwa kuwa navyo wazabuni.

Akizungumza wakati wa mkutano wa utiaji sahihi wa mkataba huo, Meya wa jiji la Mbeya, Athanas kapunga , alisema kuwa ujenzi huo ambao umekuwa ukisubiriwa kwa hamu sana na wakazi wa jiji lake pamoja na mkoa wa Mbeya kwa ujumla, unatarajiwa kukamilika baada ya mwaka mmoja na nusu na kuwa mchakato kwa ajili ya kuanza kwa shughuli za ujenzi, umeshaanza katika hatua zake za awali.

Alisema kuwa soko jipya ambalo linatarajiwa kutoa ajira kwa maelfu ya wakazi wa mkoa huo, litakuwa na hadhi ya kimataifa na ndio sababu kazi ya kumpata mzabuni atakayeendesha ujenzi huo, ilichukua muda mrefu kidogo licha ya kuwa benki ya CRDB, ilishatangaza kutoa kiasi cha shilingi za kitanzania bilioni 13, ili kufanikisha ujenzi huo.

Aliongeza kuwa, licha ya kupatikana kwa kampuni hiyo itakayofanya ujenzi, Halmashauri ya Jiji la Mbeya, kupitia wataalamu wake mbalimbali, imejiwekea mkakati wa kuhakikisha kuwa inakuwa karibu na mzabuni huyo kwa masuala ya kiushauri ili kufanikisha azma ya ujenzi huo kukamilika ndani ya muda muafaka.

Meya wa jiji hilo, alisema kuwa nia ya kutaka ujenzi huo kukamilika ndani ya muda mfupi, inatokana na ukweli kuwa, kuungua kwa soko la awali kulililetea jiji mkoa mzima hasara kubwa kimapato, hususanii katika ukusanyaji kodi, kutokana na wafanyibiashara wengi kukosa sehemu maalum za kufanyia biashara zao.

Aliitaka kampuni hiyo kuhakikisha kuwa inashirikiana bega kwa bega na Halmashauri ili kufanikisha kamilisha kazi hiyo kwa mujibu wa makubaliano, ili kufanikisha azma ya serikali ya awamu ya nne ya kuwaletea maisha bora Watanzania na hususan wakazi wa Mbeya, ambao wengi wao ni wakulima na wanaotegemea zaidi masoko kwa ajili ya kuuza mazao yao.

Awali meneja ushauiri wa ujenzi wa kampuni ya MD Architects Consulnatcy, Dudley Mawalla, aliwaeleza wageni waliohudhuria utiaji sahihi huo kuwa, kampuni yake imefurahi kushinda zabuni hiyo na kuahidi kuwa itashirikiana kwa ukaribu na uongozi wa Halmashauri ya jiji katika kukamilisha jukumu kubwa walilo nalo la kuwapatia wakazi wa mbeya eneo lenye hadhi ya kimataifa kwa ajili ya kufanyia kazi zao na kwamba litachukua wafanyabiashara 3500.

Hata hivyo, aliwataka wananchi wa Mbeya kwa ujumla kutoa ushirikiano kwa kampuni yao ili kazi hiyo iende kwa kasi iliyokusudiwa, akisema kuwa, uongozi wa Halmashauri peke yake hauwezi kufanikisha hilo ikiwa wananchi wenyewe watakuwa hawana mwamko wa kushiriki katika kufanya jambo hilo la kujiletea maendeleo.

Akitia mchanganuo wa namna watakavyofanikisha ujenzi huo, alisema kuwa tayari kazi ya kuandaa michoro ya jengo litakalojengwa imeanza rasmi Oktoba 31, na kwamba katika kipindi cha miezi mitatu ijayo, kazi ya kumtafuta mkandarasi atakayefanya shughuli ya ujenzi itakuwa imekamilika na ujenzi kuanza rasmi.

Soko la Mwanjelwa, lililokuwa moja ya masoko maarufu nchini, liliungua na kuteketea kwa moto Novemba 2006, na kusababisha hasara kubwa kwa wafanyibiashara waliokuwa wakilitumia soko hilo, ikiwa ni pamoja na maduka na vibanda zaidi ya 900 vilivyokuwa vikitumiwa na wafanyibiashara hao kuteketea na mali zilizokuwa ndani yake.

Ujenzi wa soko hilo jipya katika eneo la Mwanjelwa, unatarajiwa kuleta faraja mpya kwa wakazi wa eneo hilo, ambao wengi wao wangali na kumbukumbu za kupoteza mali zenye thamani ya mamilioni ya shilingi za Kitanzania, ingawa ni wazi kuwa hautaweza kuwaondolea kumbukumbu ya kifo cha aliyekuwa mbunge wa Tunduru, marehemu Juma Akukweti.

Marehemu Akukweti, alifariki dunia nchini Afrika Kusini Disemba mwaka huo huo, alikokuwa akitibiwa majeraha yaliyotokana na ajali hiyo ya ndege, ambayo ilimfika wakati akijaindaa kurejea jijini Dar es Salaam, baada ya kuwapa pole wahanga wa ajali ya soko la Mwanjelwa.
Share on Google Plus

About Rama Msangi

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

1 maoni:

Anonymous said...

kwakweli itabidi serikali ilitangaze eneo la Mwanjelwa kama eneo la kumbukumbu maalum ya marehemu Akukweti. Nadhani na soko lenyewe lingeitwa soko la Akukweti, kama moja ya njia za kuenzi kile kilichomtokea wakati akiwa amefika eneo hilo kuwatembelea na kuwapa pole wahanga wa soko la awali lililoungua