side ads

JK na CCM yako, usanii wenu ndio chanzo cha matatizo yenu

Nakumbuka kusoma au kusikia mahali kuwa mwanazuoni mmoja aliwahi kusema "Inapofikia mahali nchi imekwama, kwa maana viongozi hawajui wanakoelekea, basi wale waliokuwa nyuma ambao ni wananchi na hususan wale wa kada ya chini ambao ndio wengi zaidi, huamua kuchukua hatamu za kuonyesha njia iliyo sahihi"

Naam, nayakumbuka haya wakati nikiwa naungana na baadhi ya Watanzania wenzangu, ambao matukio yaliyojiri nchini mwetu katika kipindi cha takriban wiki mbili za katikati ya mwezi huu wa Oktoba 2008, hayawezi kuachwa yakapita bila kufikiriwa kwa kina.

Ktika wiki hizo tumeshuhudia chama kikongwe, na kinachoitawala Tanzania tangu enzi na enzi, CCM, licha ya uwekezaji mkubwa wa mabilioni ya fedha waliyokuwa wamewekeza katika kuhakikisha kuwa wanalitwaa jimbo hilo, ambalo katika uchaguzi wa mwaka 2005, lilitwaliwa na CHADEMA.

Ni katika wiki hizo ambapo pia tumesikia msafara wa Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM, taifa na Amiri Jeshi mkuu wa nchi hii, Bw. Jakaya Mrisho Kikwete, ukipopolewa mawe katika kijiji cha Kanga Mkwajuni, wilaya ya Chunya, mkoani Mbeya.

Ingawa CCM, sio sawa na lile chama jingine la Msimbaazi, ambalo liko katika mgogoro mkubwa hivi sasa kutokana na mwenendo wao katika ligi kuu ya Tanzania, lakini nilitarajia hivi sasa CCM, wangekuwa katika vikao vizito vya kichama kutafakari matukio hayo mawili, kulingana na uzito wake.

Badala yake, CCM, wameingia katika ule ugonjwa ambao wamekuwa wakiugua siku zote. Ugonjwa wa kupuuza, kiburi, jeuri, dharau, viini macho pamoja na kile ambacho mwandishi Deus Bugaywa, katika moja ya makala zake, alikiita 'ulevi wa propaganda za chama kikongwe'.

Tukianza na kilichotokea Tarime, nilishangaa sana kusoma katika vyombo mbalimbali vya habari kuwa kada mmoja wa chama hicho, ameshangazwa sana na matumizi makubwa ya fedha yaliyofanywa katika kampeni za uchaguzi huo. Ilinishangaza sana kwasababu siamini kuwa kada huyu, hakuwa mmoja wa waliopitisha maamuzi ya CCM, kujibu mapigo ya CHADEMA, kwa kufanya kampeni za anga kwa anga, za kutumia helikopta.

Ununuzi wa fulana zenye picha za wagombea, vitenge na khanga, hafla zinazoambatana na pilau kwa ajili ya kuwarubuni Watanzania wasiojua thamani ya kura zao, manunuzi ya shahada za kupigia kura na hata wizi wa kura, ni miongoni tu mwa mambo yenye kuigharimu fedha nyingi zilizo na zisizo halali, na ambayo tumekuwa tukisikia au kushuhudia kufanywa na chama hiki kwa lengo la kushinda.

Leo hii anapoibuka mmoja wa viongozi wake na kudai kushangazwa na uendelezwaji wa sera yao ya kichama katika uchaguzi wa Tarime, anataka kutuambia nini hasa? Unafiki au kudhihiri kwa moto wa mpasuko ambao CCM, imekuwa ikijitahidi kuuficha kwa kutumia makaratasi na nyasi zilizokauka? tuyaache hayo kwanza, twende Mbeya, ambako msafara ulipigwa mawe.

Siku ile ile ya tukio lile, mara baada ya kuwasili jijini Mbeya, mkuu wa mkoa wa Mbeya, Bw. Charles Mwakipesile, aliita waandishi wa habari na kuwaeleza eti waliurushia mawe msafara wa Raisi jioni ya siku hiyo, walikuwa ni walevi tu.

Kesho yake, Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu, akanukuliwa akisema waliofanya hivyo ni wananchi waliokuwa na shauku ya kumuona raisi wao, lakini akashindwa kusimama kijijini kwao kwasababu ya giza. Akaongeza kuwa raisi amefadhaishwa sana na tukio hilo. Vyombo vya dola navyo vikadai uchunguzi unaendelea.

Siku chache baadae, wakati Bw. Kikwete, mwenyewe akiwa anahitimisha ziara yake akasema kuwa wala hakufadhaishwa na tukio lile, na analichukulia la kawaida tu kama changamoto za uongozi. Uh!! Hapa, ndipo ninapolazimika kushusha pumzi kwanza, maana mzigo wa maswali kichwani unaniwia mkubwa zaidi kuliko majibu yanayoweza kupatikana.

Miongoni mwa maswali hayo ni, je, walioupopoa mawe msafara wa raisi walikuwa walevi au wananchi waliokuwa na hamu ya kumuona lakini wakashindwa kutokana na giza? Raisi alifadhaishwa na tukio hilo, ama alilichukulia kama changampoto za kiuongozi? Kama waliofanya hivyo wanajulikana, Polisi wanachochunguza ni nini hasa?

Na hapa ndipo ninapokumbuka maneno aliyoyaandika kaka yangu Ansbert Ngurumo, katika moja ya makala zake kuhusiana na kizaa zaa hiki akisema (nanukuu) "...Najua serikali yenyewe haiamini kauli yake, ndio maana imemwaga mashushushu mahali hapo kuchunguza sababu za kitendo hicho" (mwisho wa kunukuu)

Haishangazi sana kusikia kumwagwa kwa mashushushu ambao hatimaye gazeti moja liliripoti kuwa tayari lilishafanikiwa kukamata watu 60, na wakawa wanapungua kwa kadiri walivyokuwa wakihojiwa. haishangazi kwasababu mfumo huu wa utawala, wa kutumia vyombo vya dola kudhibiti sauti za wananchi, umekuwa ni mtindo ambao umekuwa ukizidi kuota mizizi ndani ya CCM.

Na ukijani wa mti huu unaostawishwa mbolea ya mchanganyiko wa ulevi wa madaraka, dharau, kiburi na jeuri ya utajiri wa dhuluma ambao genge fulani la viongozi walio na uchu na tamaa za kifisadi, wamekuwa wakiuchuma toka katika jasho la Watanzania ambao maisha yao yameendelea kuwa duni kila uchao.

Kwa bahati mbaya sana wanachama wa genge hili, wamefikia hatua ya kujisahau kuwa Tanzania ya sasa wanayoiongoza, haiko sawa na ile waliyokuwa wanaifikiria wakati wanapanga mikakati ya kuitumia kama kitega uchumi chao. Wamekuwa viziwi wa kusikia maonyo wanayopewa kila kukicha. wamekuwa vipofu kuona yanayojiri nchi za jirani na sisi na katika nchi ambazo ni marafiki wa Tanzania.

Fedha za dhuluma walizojilimbikizia katika akaunti zao, wanaona zinaweza kununua kila kitu. Kununua madaraka, kununua imani ya wananchi, kununua hata uwezo wa Watanzania kuyaona na kuyahisi maumivu ya makali ya maisha wanayokabiliana nayo. Naam, wanadhani fedha zao zinaweza kuifanya Tanzania ikasimama kila wanapopenda wao, ili waweze kufanya dhuluma zao tena waziwazi wakiwa wanaonekana. Inashangaza sana kwa hakika.

Ingawa sina nia na wala sitamani hata siku moja kuhubiri injili za fujo, ghasia na machafuko ya aina yoyote katika nchi hii ambayo najivunia kuwa mmoja wa wananchi wake, lakini nashindwa kujizuia kukumbuka historia ambayo inaniambia kuwa kuna mataifa ambayo wananchi wake, baada ya kuchoshwa na ukiziwi wa watawala wao, walifikia hatua ya kuchukua hatua ya kuwakata vichwa na kuvitundika minarani na kisha kujitwalia madaraka wao wenyewe.

Nashindwa kuamini kuwa CCM, bado iko katika mning'inio wa ulevi wa sifa ambazo walinyweshwa na viongozi wa kidini ambao mwaka 2005, walituhubiria kile walichokiita 'Chaguo la Mungu kwa Watanzania' na wale wanahabari wenzangu ambao wakati fulani walitumia jitihada kubwa kuwafanya Watanzania waamini kuwa, Masiha, alikuwa amerejea, tena amefufukia Tanzania, ili kuwakomboa Watanzania.

Nashindwa kuamini kuwa JK na CCM yake, wameshindwa hata kushtuka katika usingizi mzito waliolala, hata baada ya kuonyeshwa vibatari, ndoo za maji, mikutano kuingiliwa na matrekta, kupigwa mawe magari yanayotangaza ujio wa viongozi wa ngazi za juu na matukio mengine ya namna hiyo.

Lakini ni vyema CCM, ikakumbuka kuwa, mara zote, uvumilivu huwa una ukomo wake. Ni vyema ikakaa na kuitafakari hali hii ya matukio ya kuwaaibisha viongozi wakuu wa nchi, kuliko kutumia nguvu kubwa katika kucheza mchezo wa kijinga wa kukanusha ukweli. Ukweli huwa haupingwi hata siku moja. Ukweli ni sawa na moto ambao hauwezi kufunikwa au kufichwa kwa makaratasi au nyasi kavu.

Ni vyema CCM, ikajiuliza kuwa baada ya matukio ya Tarime, Mwanjelwa, Uyole, Kanga, Manyara na kwingine, kitakachofuata ni nini? Ni vyema ikajua kuwa licha ya kumiliki na kuwa na umahiri wa kuvirubuni na kuvitumia vyombo vya dola, wananchi wanaposema kuwa wamechoka, humaanisha wamechoka kweli na huwa hawaogopi risasi au bomu la aina yoyote ile.

Nashawishika kusema kuwa, kuna baadhi ya viongozi ambao wanawasukuma Watanzania katika kile wasichokitamani, kuonja ladha ya machafuko ndani ya nchi yao.

Nashawishika kusema kuwa kuna baadhi ya viongozi ambao kutokana na kujilimbikizia mali kwa wingi kwa kudhulumu jasho na haki za Watanzania, wameona kuwa njia muafaka ya wao kuweza kuikimbia nchi ni kuandaa mipango ya machafuko, kwa kuwapora kila kilicho chao Watanzania, huku wakiziba masikio wasisikie kilio chao na kuivuruga nchi, ili wapate kisingizio cha kuikimbia nchi hii.

Na kama wapo watu wenye fikra za namna hii, ni vyema wakajua kuwa wamechelewa sana, kwa maana kila mtenda dhambi, hulipwa humuhumu dunaini hata kabla hajafika kwa Mungu. Mtalipwa hapahapa duniani hata kabla mnayodhamiria hayajatimia.

Halahala jamani, fumbeni macho zibeni masikio, vuteni shuka na endeleeni kukoroma usingizi wa dhuluma, nasi tukiamua kuwaamsha......... tusijeonana wabaya
Share on Google Plus

About Rama Msangi

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

1 maoni:

Mzee wa visa said...

Kamanda, nimekaminia. Hii kazi ya kuiboresha blogi yakoimekuchukua siku ngapi? Du!! umekamata mshkaji. Nimekunyooshea mikoo kwaweli. Saluti...saluti...saluti kamanda