side ads

HAPA MWANZO

MISUKOSUKO ya kimaisha, ni sehemu muhimu sana ya uhai na kuishi kwa mwanadamu. na kifupi ni kuwa, hakuna mwanadamu ambaye hajawahi kuwa katika NJIA PANDA ya au za kimaisha.

Kulia, kusononeka, kuumizwa, kufurahishwa, kuudhiwa, kukata tamaa, kufanikiwa, kuanguka kimaisha na mengineyo ya namna hiyo, ni hatua ambazo kila mwanadamu lazima azipitie katika safari yake ya maisha.

Wataalamu wa masuala ya mienendo ya maisha, na hata maandiko matakatifu, hutueleza kuwa, kwa kadiri mwanadamu anavyokumbana na changamoto nyingi za kimaisha, ndivyo anavyozidi kuimarika kiakili, kimwili na kiroho.

Kila mmoja wetu, kwa namna moja ama nyingine, ameshakumbana na moja ya changamoto zilizokuwa kubwa na ngumu sana katika maisha yake. Na kila mmoja wetu, alishawahi kuzikabili kwa njia mbalimbali ambazo wengine hawazijui.

Hata hivyo, moja kati ya njia ambazo zimekuwa za manufaa sana katika kujaribu kupunguza ugumu wa kazi ya kukabiliana na changamoto za kimaisha, ni ile ya kupata ushauri ulio mzuri wa namna ya kukabiliana na nyakati hizo zilizo ngumu za kimaisha, toka kwa marafiki ambao walishakumbana nazo.

Kubadilishana uzoefu wa kimaisha na marafiki ambao nao walishawahi kupitia changamoto mbalimbali, kumewasaidia wengi wetu kuweza kujiweka katika hali nzuri ya kuweza kukabiliana na nyakati ngumu zinazotutokea katika maisha yetu katika kipindi cha uhai wetu.

Kwa muda mrefu sana, nimekuwa mmoja kati ya watu wanaoabudu falsafa hii ya majadiliano hasa ya kubadilishana uzoefu wa kimaisha, kama njia nzuri ya kuniwezesha kukabiliana na changamoto za kimaisha na pia kuniweka katika hali inayoniwezesha kukabiliana na jambo pindi litakaponitokea.

Ninawashukuru sana wale wote walio marafiki zangu, ambao kwa nyakazi zote za shida na raha, mmeweza kuwa karibu sana na mimi. Mkinishauri, mkinipa mwongozo na kunipa moyo wa yale yaliyokuwa magumu yakinikabili.

Nawashukuru sana marafiki zangu ambao, tumekuwa tukibadilishana uzoefu wa masuala mbalimbali ya kimaisha. Aidha, ninawashukuru zaidi wale ambao kupitia maongezi yetu, mliweza kunufaika na mawazo na mchango wangu katika kuwasaidia kukabiliana na changamoto za kimaisha. Na hii, ni maalum kwenu ninyi.

Njia panda za maisha, itakuwa ni blogi maalum kwangu mimi, marafiki zangu, wasomaji wa blogi zangu za Uchambuzi, yenye kuzungumzia masuala ya kijamii kwa ujumla, na ile ya Nilichokiona, iliyo maalum kwa ajili ya picha mbalimbali.

Ni maalum kwa wale wote ambao wamekuwa wanakabiliwa na changamoto mbalimbali za kimaisha ambao wamekuwa wakihitaji msaada wa kiushauri lakini wakawa hawana pa kuupata. Ni kwa wale ambao wamejaaliwa kipaji cha kuweza kuwashauri wengine wenye matatizo lakini wakakosa nafasi ya kuweza kufanya hivyo.

Njia panda za maisha, ni blogi yangu mpya ambayo itakuwa na lengo la kutoa mafundisho mbalimbali kwa ajili ya kila anayeisoma kuweza kujua njia na mbinu mbalimbali za kukabiliana na changamoto za kimaisha. Ni sehemu maalum ambayo nitapenda marafiki zangu wasaidiane na mimi katika kuwasaidia wale ambao wako katika shinikizo kubwa sana la kimaisha.

Ni blogi ambayo itakuwa ikiainisha njia mbalimbali ambazo mwanadamu anaweza kuzitumia au kuzipitia katika kipindi anachokuwa anakabiliwa na tatizo fulani, ili aweze kuondokana nalo. Ni blogi ambayo imelenga katika kusaidiana, kuonyeshana na hata kuongozana katika upande ulio sahihi zaidi, pale unapokuwa katika njia panda za kimaisha.

Nawashukuru sana marafiki zangu ambao mliona kuna umuhimu wa kuwa na blogi ya aina hii, mkanishauri niianzishe, na nataraji mchango wenu sana katika kufanikisha blogi hii. Nawashukuru kwa kuvumbua na kunijulisha kuwa nina uwezo wa kufanya jambo kama hili.

Ingawa si rahisi kuwataja marafiki zangu wote katika sehemu hii, na hasa kwa kuwa pia sijapata idhini ya kuwataja kila mmoja wao, basi ni vyema tu niseme kuwa naamini shukrani zangu zitawafikia popote mlipo, kwakuwa kila mmoja wenu yuajijua kuwa alinishauri kipi. Asanteni sana

Kwa pamoja tutaweza, kwa pamoja tutatoka katika njia panda za maisha.
Share on Google Plus

About Rama Msangi

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni: