side ads

FUJO ZA MSAFARA WA JK MBEYA.. CHA KUSHANGAZA KIPI?

Walikuwa na hamu ya kuonana na kuongea na raisi, lakini ikashindikana
kwasababu tayari ilishakuwa usiku sana, walikasirika na kurusha mawe
kwakuwa walikosa fursa ya kuonana na kiongozi wao. Raisi amesikitishwa sana na tukio lile


Hayo ni maneno yaliyonukuliwa kusemwa na Ofisa habari na Mawasiliano wa Ikulu, Bw. Salva Rweyemamu, akielezea tukio la msafara wa Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kushambuliwa kwa mawe na baadhi ya wakazi wa kijiji cha Kanga Mkwajuni, wananchi wilayani Chunya.

Hata hivyo, wakati Bw. Rweyemamu, akilitolea hilo ufafanuzi, halikuwa tukio la kwanza la msafara wa Raisi Jakaya Kikwete, kufanyiwa fujo, akiwa katika ziara yake ya siku kumi ya kikazi katika mkoa wa Mbeya.

Katika siku za mwanzo wa ziara hiyo, alikumbana na tukio la msafara wake "kuvamiwa" na wananchi waliozuia barabara eneo la Kabwe, jijini Mbeya, kisha kukumbana na hali kama hiyo eneo la Uyole, pia ndani ya jiji la Mbeya.

Nasikia waandishi walioyaona matukio hayo kuwa ni habari, eti waliulizwa "Hamkuona habari nyingine za maana za ziara hii hadi matukio hayo yawe habari?" Anyway, tuwaachie hayo.

Ingawa wapo watakaoshangaa, lakini ni vyema nikiri kuwa, yote yaliyoutokea msafara wa Raisi, nilitaraji kuwa yangetokea, ingawa sikujua ni kwa mtindo gani. Ndio, niliyatarajia kwasababu viashiria juu ya uwepo wa matukio haya, vilikuwepo vya kutosha tu.

Tumesahau kuwa mheshimiwa JK, alishakumbana na kadhia ya wananchi waliompokea wakiwa wamebeba madumu ya maji na ndoo, wakiashiria kukabiliwa na shida ya maji. Si alishawahi kupokelewa na wananchi kwa vibatari, wakiashiria matatizo ya nishati?

Tumesahau wale makada wa CCM, ambao mkutano wao wa kuhanikiza 'mafanikio ya ilani ya CCM', ulivamiwa na mkulima aliyeingia na Trekta lake katika viwanja vya CCM, Ilomba, kama ishara ya kutokukubaliana na kile walichokuwa wakidai mafanikio katika kilimo?

Tumesahau gari lililokuwa likitangaza ujio wa Raisi, kipindi fulani huko nyuma, kupigwa na mawe katika eneo la Mwanjelwa? Taarifa ambazo uongozi wa mkoa wa Mbeya, haukuzichukulia kama dalili mbaya na wakawekeza nguvu zao katika kuzipinga badala ya kuangalia kuwa ziliashiria nini?... kwa hali hii, hakika niliyatarajia yaliyoukumba msafara wa raisi.

Hayo ni baadhi ya mambo yanayojenga msingi wa imani yangu kuwa matukio ya fujo, uvamizi, mashambulizi na vingine utakavyoita, yaliukumba msafara wa raisi mkoani Mbeya, niliyatarajia. Kwakuwa yalishatokea, kuyajadili si issue tena, na badala yake labda ni vyema kuangalia sababu za msingi za matukio hayo.

Katika historia ya nchi hii, ambayo niliisona toka shule ya msingi hadi sasa, tukio la msafara wa raisi kushambuliwa kwa mawe, limetokea kwa mara ya kwanza katika awamu hii ya nne ya utawala chini ya mheshimiwa JK. Na kwa imani yangu, hata tukio la raisi kusimamishwa na wananchi na kisha kupigiwa kelele za "Ufisadi...Ufisadi...Ufisadi...", limetokea kwa mara ya kwanza katika awamu hii hii.

Hili si jambo la kujivunia kwa Raisi ambaye aliingia madarakani kwa 'Ushindi wa...kishindo (au ulikuwa wa kimbunga vile?). Raisi ambaye aliingia madarakani kwa mbwembwe na ahadi nyingi. Raisi, ambaye nyuma yake kulikuwa na imani kubwa sana ya wananchi waliomchagua.
Ni nini basi kimemkumba mtu huyu ambaye baadhi ya viongozi wa kidini walithubutu kutumia majumba ya ibada na majukwaa mbalimbali kudai "Jakaya Kikwete ni chaguo la Mungu" Ni ufisadi, majungu, umbea, uzushi au chuki binafsi? Je, ni rushwa, uchochezi wa kisiasa, kutokufikiwa kwa matarajio, kutotimia kwa ahadi zake kwa watanzania au ni nini hasa?

Naam, ziko sababu nyingi sana kwa hakika, kwa maana ukiachilia mbali hizo hapo juu, zipo nyingine kadha wa kadha. Na karibu kila mtu ana sababu zake ambazo ni za msingi sana. lakini kwa pamoja tu, ni vyema tukaziweka sababu zote hizo katika kapu moja ambalo linazikusanya kwa pamoja, nalo ni MFUMO MBOVU WA KIUTAWALA, ambao serikali ya awamu ya nne ulijiundia.

Ni bahati nzuri sana kuwa, hadi wakati anaingia madarakani, mheshimiwa JK, alikuwa ni mmoja kati ya waliokuwa wanaonekana watu wasafi na wasiokuwa na doa katika zama za utawala huko mwanzo walikokuwa wamepitia. Na bahati nzuri zaidi ni kuwa hakuwa ameipata sifa hiyo kwa kusingiziwa. Aliistahili.

Ndio, aliistahili, kwasababu katika karibu sehemu zote ambako alikuwa amepitia na kuongoza kabla hajaukwaa uheshimiwa namba moja mwaka 2005, mheshimiwa Kikwete, alijitahidi sana kuongoza sehemu hizo kwa kuzingatia utashi wa kitaaluma, pamoja na mahitaji ya sehemu hizo na yale ya Watanzania.

Bahati yake mbaya sana ni kuwa, alianza kuharibu mambo wakati alipokuwa katika harakati za kuingia Ikulu. Na kosa la kwanza lilikuwa lile la kugawa chama katika makundi maarufu kama mitandao, kama ilivyokuwa ikijulikana. Sina hakika sana kama hakujua uzito wa jambo alolikuwa amelifanya wakati huo, lakini jambo moja nililo na hakika nalo ni kuwa tamaa ya Ikulu, ilikmpofusha na kumfanya kiziwi.

Hakuweza kuona madhara yake mbeleni, na wala hakuweza kusikia kelele alizokuwa akipigiwa kuonywa juu ya mitandao aliyokuwa akiiunda. Na matokeo yake yalianza punde tu baada ya kuingia Ikulu, ambapo naamini alilazimika kugawa vyeo kwa kuzingatia mahitaji au shinikizo la Wana-Mtandao.

Pengine hilo lisingeweza kuwa tatizo kubwa sana, kama asingefanya kosa la pili ambalo naamini ndio kosa kubwa sana ambalo kwakuwa naamini yeye ni muungwana, analijutia, japo kichini chini, akiumia rohoni mwake. Hili lilikuwa kosa la kuongoza kwa misingi ya kisiasa badala ya misingi ya uongozi ambayo aliitumia awali na kumjengea sifa kubwa.

Miongoni mwa mambo ambayo aliyaahidi siku anazindua Bunge, ilikuwa ni pamoja na kuwashughulikia viongozi wote wazembe, mafisadi, na kuhakikisha maisha ya kila mwananchi yanaboreka. Na ingawa kujiuzulu kwa swahiba wake wa karibu aliyekuwa Waziri Mkuu, limekuwa kama moja ya silaha ambazo zinatumika kujinasibu kuwajibisha viongozi wazembe, lakini ukweli ni kuwa hali ni kinyume kabisa.

Mapungufu ya kiuongozi katika karibu kila idara, bado ni tatizo kubwa kuliko linavyosemwa midomoni mwa wanaolisema. Zama za uongozi ambao ni sawa na miungu watu zimejionyesha wazi wazi katika kipindi hiki, na hususan katika ngazi za chini za kiutawala ambazo kimsingi ndio zilizo karibu kabisa na wananchi.

Tatizo la mafisadi, limekuwa kubwa sana katika zama hizi, huku pengo baina ya masikini na matajiri likizidi kukua kila uchao. Juhudi za kupambana na mafisadi hata wale ambao wameshabainishwa wazi wazi, zimekuwa zimelenga zaidi katika porojo za kisiasa zaidi kuliko uhalisia. Hadi kufikia wakati wa kupewa hata muda wa kurejesha fedha walizoiba.

Haya yanatokea wakati katika kada ya wananchi wa chini kabisa, walio masikini sana, wizi wa kuku ni kosa ambalo limekuwa likimfunga mtu huyo, hata bila ya kupewa fursa ya kutafuta fedha kwa ajili ya kulipia kuku huyo. Bila hata kujua kuwa huenda mtu huyo njaa ndio ilimsukuma kuiba ama ni tabia yake ya kawaida.

Hali inazidi kuwa mbaya sana katika zama hizi ambako, wakati hali za wananchi zikizidi kuwa mbaya, uwekezaji katika masuala ya kisiasa, umekuwa ni wa hali ya juu pengine kuliko zama zozote ambazo nchi hii imezipitia. Mikutano mingi imekuwa ni ya kujadili zaidi masuala ya kisiasa badala ya matatizo ya wananchi. Hata katika vikao vya kimaendeleo, siasa zimekuwa zikijengewa mazingira ya kutawala zaidi kuliko mijadala husika.

Kwa upande wa mkoa wa Mbeya, kwenyewe ambako matukio hayo ya kushtusha yametokea, hali ni zaidi ya mbaya. Malumbano ya kisiasa yaliyotokana na mpasuko ndani ya CCM, ambao chanzo chake kilikuwa harakati za kuwania uraisi mwaka 2005, ndio jambo pekee ambalo wananchi wa mkoa huo, wanaloweza kujivunia toka awamu hii ianze.

Misuguano ya chini chini na hata ile ya waziwazi, ni jambo ambalo hakuna mwananchi ambaye halijui. Na licha ya kuwepo kwa viini macho vya hapa na pale kuhusu kuipatia mogogoro hiyo suluhu, ukweli umeendelea kubaki palepale kuwa hali si shwari ndani ya uongozi wa CCM mkoani hapa. na mheshimiwa JK, akiwa kama mwenyekiti wa CCM kitaifa, anaonekana kama ameshindwa na tatizo hili.

Ni kutokana na ukweli huo, ndio maana wananchi ambao wanaona kuwa kila nguzo yao ya kuegemea imeota miba na hawawezi kuegemea, wanaona suluhisho pekee ni kuonyesha hasira zao waziwazi kwa kila ambaye wanaona kuwa anastahili kufikishiwa hasira zao. na yaliyokwishatokea Mbeya, yanaweza kuwa mwanzo tu, wa matatizo zaidi, ikiwa serikali haitaona umuhimu wa kukaa na kujipanga upya kukabiliana na kero za wananchi.

Tiba iliyo bora sana katika ugonjwa wowote ule, ni kuanza kukiri ukweli kuwa tatizo hilo lipo, ili kuweza kukabiliana nalo. CCM, JK na safu yako nzima ya uongozi, ni vyema mkakiri kuwa hali si shwari. Mmeteleza na mko katika njia iliyo mbovu sana, nyembamba pengine kuliko uzi wa kushinea nguo, na msipokuwa makini............. sipendi kusema zaidi ya hapo.

Share on Google Plus

About Rama Msangi

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni: